Na Asha Mwakyonde,Dar es Salaam
KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kwenye maeneo ya gesi asilia ambapo amesaidia na anaendelea kufuatilia kutoa leseni kwa wale wanaojenga vituo hasa vya gesi iliyokandamizwa (CNG), pamoja na vituo vya mafuta.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mhandisi Mramba, alipotembelea banda la EWURA katika maonesho ya 48 ya Kimataiafa ya Biashara Dar es Salaam (DITF),amesema Mamlaka hiyo inasimamia na kuhakikisha huduma zinazotolewa na vile vituo vinakidhi mahitaji ya jamii.
Mhandisi Mramba huyo ameeleza kuwa jukumu la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha kwamba EWURA inafanya kazi yake kulingana na sheria na sera zilizopo na kwamba wanaiwezesha kutekeleza majukumu yake katika mazingira yanayokubalika ndani ya sekta.
"Tunaendelea kuwatia moyo watanzania kuwa zipo huduma za kiushauri ambazo EWURA inazitoa, zipo huduma za kusikiliza malalamiko na kuyafanyia kazi, amesema Mhandisi Mramba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA James Andilile amesema Mamlaka hiyo imeingia mkataba na Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), kwa lengo la kusimamia utendaji kazi wao ili kuboresha utendaji huo na upatikanaji wa umeme .
Ameongeza kuwa kwa sasa Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Nishati ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarika.
0 Comments