Dar es Salaam
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt.Dorothy Gwajima amesema Taasisi ya uhisani ya Merck Foundation inayojishughulisha na Huduma za Jamii, inatarajia kufanya mkutano wake wa 11 nchini Tanzania tarehe 29 na 30 Oktoba 2024 jijini Dar Es Salaam.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Septemba 18, 2024 jijini Dar Es Salaam.
Amebainisha kwamba, Mwenyekiti wa mkutano huo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema, kufanyika kwa Mkutano huo nchini kwa mara ya kwanza, kunatokana na Rais Samia kuridhia ombi la Taasisi hiyo.
Waziri Dkt. Gwajima amesema Taasisi ya Merck Foundation ilipendekeza kufanya Mkutano huo nchini Tanzania kutokana na jitihada za wazi za Serikali, kuwekeza katika sekta ya afya, hasa afya ya akina mama na watoto, ambavyo vimeifanya Tanzania kufanya vizuri katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kimataifa yakiwemo ya Milenia na Maendeleo Endelevu.
Waziri Dkt. Gwajima ameendelea kusema Mkutano huo unaratibiwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Merck Foundation na utahudhuriwa na Wenza wa Marais kutoka nchi 22 za Afrika na mwenyeji Tanzania, ambapo Mwenza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mariam Mwinyi atawakilisha.
Mkutano utahudhuriwa pia na Mawaziri wa Afya, Jinsia, Mawasiliano, Elimu, Ustawi wa Jamii kutoka nchi zilizoalikwa, Wataalam wa huduma za afya 500, wasomi, watunga sera, Mabalozi, waandishi wa habari na Wajumbe wengine takribani 500 kutoka sehemu mbalimbali za dunia watashiriki kwenye Mkutano kwa njia ya mtandao.
Ameendelea kueleza kuwa, pamoja na mambo mengine mkutano huo utajadili mada nne za kitaalamu kuhusu Afya ya Mama na mtoto, ugonjwa wa Saratani, ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la damu. Mada nyingine ni mafunzo kwa vyombo vya Habari kuhusu Mipango ya Maendeleo na kujengewa uwezo.
Mkutano huo pia utatumika kama jukwaa la kuchukua hatua mahususi katika kushughulikia unyanyapaa na mtazamo wa kijamii wa utasa, kuboresha upatikanaji wa huduma ya uzazi salama iliyodhibitiwa, na yenye ufanisi kwa wanawake na wasichana Barani Afrika.
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, washiriki wa Mkutano huu watanufaika na maarifa na uzoefu unaotolewa na wataalam mbalimbali na watafiti ambao watazungumza kwa kina kuhusu mada tajwa hapo juu kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii juu ya masuala mbalimbali ya afya ikiwa ni pamoja na Magonjwa yasiyoambukiza, matatizo ya kupumua, na mengineyo.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, ambavyo ni tunu za taifa na sumaku kwa wadau mbalimbali wanaofika nchini kwa ajili ya shughuli za utalii, ukiwemo wa mikutano na kujitokeza kuwania fursa mbalimbali zitakazoenda sambamba na uwepo wa wageni katika Mkutano huo.
0 Comments