Na WMJJWM, Kilimanjaro
WAZIRI wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba amewataka Wataalam wa Ustawi wa Jamii mchini kwa kushirikiana na wadau kuandaa na kutekeleza mkakati wa kuwaondoa Watoto wanaoishi na kufanya Kazi Mitaani ngazi ya Taifa.
Maelekezo hayo yametolewa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii Septemba 18, 2024 mjini Moshi, mkoa wa Kilimanjaro.
Mhe. Chande amesema mkakati huo uendane na mpango wa ufuatiliaji na mikakati itakayoandaliwa ngazi ya Mikoa na Halmashauri, huku Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na wadau kuendelea kutoa elimu ya malezi chanya kwa jamii ili kuwa na nguvu kazi yenye tija kwa Taifa.
Amewaasa pia Maafisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu kwa kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
"Mikoa na Halmashauri muandae na kutekeleza Mpango mtambuka wa kuzuia na kushughulikia ukatili dhidi ya watoto, ukatili wa kijinsia na tatizo la Watoto Wanaoishi na Kufanya Kazi Mitaani utakaojumuisha kutengeneza nyaraka ya mkakati wa Mikoa ambayo taarifa yake itawasilishwa kwenye vikao vya Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Mikutano ya Wataalam wa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Biashara, Sheria, Kilimo, Utalii, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi, Makamanda wa Mikoa" amesema Mhe. Chande.
Aidha,mewaahidi wataakam hao kulifanyia kazi suala la kuweka afua ya Ustawi wa Jamii na kuainisha kwenye Mwongozo wa Bajeti kwa Mwaka 2025/26 kama zilivyoainishwa afua zingine na kuweka mgao wa 3% ya bajeti ya kutekeleza.
Ameziomba pia Ofisi za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha zinatenga Ofisi za Ustawi wa Jamii zenye vyumba vya kutosha kutoa huduma kwa kuzingatia faragha, kuanzisha huduma ya nyumba salama kwa ajili ya kuhifadhi wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na kuendelea kuimarisha utambuzi na usajili wa Watu Wenye Ulemavu ili kuwezesha utoaji wa huduma stahiki.
Kuhusu Elimu kwa Umma, amesema kila Halmashauri iandae na kutekeleza mpango na huduma mkoba kwenye jamii na Mkoa kutoa taarifa ya kila robo mwaka kwenye Mamlaka husika na wakati wa mkutano wa mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamìi, Jinsia na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amesema Serikali itaendelea kusuluhisha migogoro ya ndoa kupitia Baraza la usuluhishi, jumuiya, kata pamoja na Maafisa Ustawi wa jamii katika mamlaka za serikali za mitaa.
Mhe. Mwanaidi ametoa takwimu za migogoro 74349 ya ndoa iliyotatuliwa ambapo mashauri ya ndoa na matunzo ya watoto 49, 302 sawa na asilimia 14.7 , yaliyatuliwa, matunzo ya watoto nje ya ndoa 25017 sawa na asilimia 18.1 yaliyoripotiwa na yaliyo mahakamani ni 4,551.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii Fatma Toufiq amewapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii kwa kufanya kazi karibu na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali bila kujali changamoto mbalimbali wanazozipitia katika kutekeleza majukumu yao ya kutoa elimu kuhusu ukatili katika jamii.
Amesema hali ya ukatili inazidi kwenye jamii hivyo kuna kila sababu ya kujiuliza tumekosea wapi mpaka vitendo vya ukatili vinazidi? . Ameongeza kuwa
wataendelea kuishauri Serikali kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kuwalinda watoto.
0 Comments