WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, UONGOZI WA TLS WAKUBALIANA KUSHIRIKIANA


Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza katika kikao na Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS), Mtumba jijini Dodoma Septemba17,2024 katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria.

Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Eliakim Maswi akiongoza majadiliano ya wataalam baina na menejimenti ya Wizara na uongozi wa Baraza la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS),kabla ya kumkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria Profesa . Palamagamba Kabudi.

Rais wa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS), Boniface Mwabukusi akielezea kufurahishwa kwake na mapokezi tangu waliowasili wizarani hapo kabla ya kuanza kuelezea hoja za ushirikiano.

Baadhi ya viongozi kutoka Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) wakifuatilia majadiliano katika kikao hicho.

Menejimenti ya Wizara na Uongozi wa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS), waliohudhuria katika kikao hicho wakifuatilia majadiliano.


Waziri wa Katiba na Sheria, Menejimenti ya Wizara na Uongozi wa Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS), wakiwa katika picha ya pamoja.

Lusajo Mwakabuku na Hyasinta Kissima ,WyKS Dodoma

BARAZA la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) likiongozwa na Rais wa Chama hicho Boniface Mwabukusi wamekubaliana kwa pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Waziri mwenye dhamana Prof. Palamagamba Kabudi kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yote yanayohusu sekta ya sheria kwa kuzingatia mipaka na taratibu kwa maslahi mapana ya Taifa.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kikao cha majadiliano kilichofanyika leo kwa zaidi ya saa sita katika katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Wizara yaliyopo Mtumba Jijini Dodoma Septemba17, 2024 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka TLS huku Wizara ya Katiba na Sheria ikiwakilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria na menejiment yote ya wizara.

Katika kikao hicho hoja mbalimbali ziliibuliwa na kutokana na uzito wa majadiliano hayo, Waziri Kabudi alielekeza Baraza hilo la TLS likae kwanza na menejimenti ya wizara ikiongozwa na Katibu Mkuu Eliakim Maswi kwa lengo la kujadili masuala ya kitaamu na baada ya hapo ikafuatia awamu ya pili iliyomjumuisha Waziri.

Hoja mbalimbali ziliibuliwa katika kikao hicho moja wapo ikiwemo utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign – MSLAC) ambapo TLS waliitaka Wizara iwahusishe wanachama wengi zaidi wa chama hicho waliopo katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwa na mwendelezo wa huduma mara kampeni inapomalizika eneo husika. 

Waziri kabudi alikubali ombi hilo na kuagiza iundwe kamati ya pamojaitakayojumuisha wanachama wa TLS na kuangalia namna bora zaidi ya kuboresha utekelezaji wa kampeni hii.

Aidha jambo la pili lililojadiliwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi (Arbitration Center) ambachokitakuwa chombo cha kimataifa ambacho kitaweza kuhudumia watu wa nchini na kutoka mataifa mbalimbali. Na hili pia Waziri akaelekeza iundwe kamati na uandaliwe mpango mzuri juu ya uanzishwaji wa kituo hiki.

Katika hatua nyingine, Rais wa Chama hicho Mwabukusi ameiomba wizara kupitia taasisi zake hasa Tume ya Kurekebisha Sheria kuhakikisha TLS inashirikishwa katika kutoa maoni katika miswada mbalimbali kabla ya kufanywa kuwa sheria lengo ni katika kuhakikisha wanakuwa na sheria bora zaidi za kusaidia wananchi. Jambo ambalo Waziri Kabudi, kama ambavyo alikubali hoja zingine na hiyo aliikubali.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa kikao hicho, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi amesema anaamini kuwa huo ni mwanzo mzuri kwani wamekuwa na kikao kizuri chenye majadiliano marefu ya staha ambapo mambo mengi mazuri yenye kustawisha demokrasia yan chi na ustawi wa jamii kupitia sekta ya sheria yamejadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake Rais wa TLS Mwabukusi amesema amefarijika kwa kiasi kikubwa kwanza kwa mapokezi ya heshima waliyopewa tangu walivyopokelewa wizarani hapo na namna mjadala ulivyoendesha huku akisema ho ni mwanzo mzuri na wanatumaini kwa kusikilizana huku basi masuala mbalimbali yanayowahusu wananchi kisheria yatapatiwa ufumbuzi.

Hiyo ilikuwa ni ziara ya kwanza ya Rais wa TLS Bwn. Boniface Mwabukusi kufika Wizarani kwa lengo la kujitambulisha tangu ateuliwe kuwa Rais Mwezi uliopita lakini kuwasilisha hoja mbalimbali za kiutendaji ambazo anadhani ni muhimu TLS na wizara wakashirikiana.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI