CHATANDA AZINDUA UWAWAMA DODOMA, AITAKA SERIKALI KUTOVUMILIA HALMASHAURI ZITAKAZOENDA KINYUME NA TARATIBU ZA UTOAJI MIKOPO


Na Asha Mwakyonde DODOMA 

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT),Mary Chatanda amesema kuwa umoja huo unaishauri Serikali kutoivumilia Halmashauri yoyote nchini ambayo haitatekeleza kwa uadilifu zoezi la utoaji Mikopo ya asilimia kumi.

Mwenyekiti huyo ameasema hayo leo Novemba 1, 2024 jijini Dodoma wakati akizundua kikundi cha Umoja wa Wanawake wafanyabiashara Masoko (UWAWAMA).

Amesema kuwa mikopo hiyo ni haki ya kila Mtanzania, huku akisema Wanawake wamepata bahati kubwa ya kupewa kipaumbele ambapo anawawahimiza kuchangamkia fursa ya mkopo usio na riba wanayopewa na Serikali kwa lengo la kuondokana na mikopo ya Kausha damu, ujinga na mwendokasi inayo wanyanyasa na kuwadhalilisha Wanawake kutokana na utaratibu wa mikopo hiyo.

Chatanda amefafanua kuwa muda wa marejesho na kiwango cha riba cha mikopo hiyo kuwa kikubwa hivyo badala ya kujikwamua kiuchumi inaongeza umasikini zaidi.

Amesema kuwa kipekee amefurahishwa kwa moyo wa uthubutu wa Wanawake hao kwani wameonesha utayari wa mabadiliko katika sera ya uchumi huku akisema watambuka, katika Kongamano la Aprili 05, 2024 lililofanyika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Conversion lilikusanya wafanyabiashara wanawake wa mbogamboga na kupatiwa mafunzo na ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kwa lengo la kuelezana takwimu za wanawake kwa kuhusishana na ushiriki katika kujenga uchumi wa nchi yetu.

 "Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anawasalimu sana anatambua kazi kumbwa mnazofanya za kuimarisha uchumi wa Familia na Taifa kwa Ujumla anawapongeza sana kwa jitihada zenu, niwaombe mpokee salaam hizo," amesema.

Aidha amewashukuru wanawake wote nchini kwa kuitikia wito wa Serikali kwa kushiriki katika zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Mkazi litakalotumika kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwezi Novemba, 27 2024, ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri anayesimamaia Uchaguzi huu (TAMISEMI) inaonesha wanawake walioandikishwa ni asilimia 51.29 na asilimia 48.71 ni wanaume.

"Asanteni sana wanawake kwa kuiheshimisha Serikali, Kiongozi wetu mkuu wa Nchi Dk. Samia pamoja na mimi Mwenyekiti wenu, ambaye wakati wa ziara zangu zote nimekuwa nikiwasihi wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha," amesema. 

Mwenyekiti huyo amewataka Wanawake kujitokeza kugombea nafasi zote Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe mchanganyiko na wale wa viti Maalum. Nawapongeza wale wote waliothubutu kugombea kupitia Vyama vyenu na kuteuliwa na ambao hawakubahatika wasikate tamaa.

"Kwa umuhimu wa kipekee naendelea kuwaomba wanawake na wananchi baada ya michakato ya uchaguzi inayoendelea, twendeni tukashiriki kupiga kura Oktoba 27, 2024, kwani uchaguzi huu ni muhimu kwa kila mwananchi kushiriki kuchagua viongozi wa Mitaa,Vijiji na Vitongoji kwani ndio viongozi wetu wa kwanza pindi tunapohitaji huduma ya Serikali," amesema.

Awali Waziri wa Madini ambaye pia ni mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde amesema kuwa atawasaidia kupata ofisi kikundi hicho na kuwalipia koda ya miaka mitatu pamoja na Pia kuwakabidhi shamba la zabibu ambalo tayari lina zabibu katika eneo la Mpunguzi

"Nimesikia mmefungua akaunti ya kikundi chenu nitawachangia milioni 10 ili muanze nayo," ameeleza Mavunde.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais Dk. Samia kwa kufanya wanawake wajiamini na kutembea vifua mbele kwa kuleta hamasa kwa wanawake kujiamini kufanya mambo makubwa ambayo anayafanya.

Amesema Rais ameendelea kuwezesha mazingira ya masoko ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara kwa uhuru na kwamba Serikali ya Rais imerejesha mikopo ya asilimia 10 kwa utaratibu ulipboreshwa.

"Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa kuanzisha umoja wenu na mkifanya vizuri na wengine watajifunza kupitia nyie," amesema.

Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza wanawake kuchanguamkia mikopo hiyo na kuanachana na ile ya kausha damu ambayo inawadidimiza kiuchumi kutokana na riba kubwa.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU