Na WMJJWM-Dodoma
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amewaasa vijana balehe wote nchini kuzingatia uadilifu katika kila yote wanayoyafanya ili waweze kufikia malengo yao na kujenga taifa imara.
Ameyabainisha hayo alipokua akihitimisha Mkutano wa wadau wanaotekeleza afua za vijana balehe nchini (NAIA) Novemba 01,2024 jijini Dodoma.
Wakili Mpanju amefafanua kwamba vijana ni nguzo imara kwa maendeleo ya taifa hivyo wanatakiwa kuhakikisha wanajilinda na kujitunza ili wasipotoshwe na maafundisho kutoka tamaduni za kigeni.
“Mnapaswa kuwa waadilifu katika kila mnachokifanya kwa kuwa mstari wa mbele kuwabainisha wale wote wanaojitokeza kuwafundisha maadili yasiyofaa katika makuzi yenu kwa kutoa taarifa katika vyombo husika kwani kuna baadhi ya mafundisho yatawapotosha na kuwapoteza“ amesema Mpanju.
Sambamba na hilo, Wakili Mpanju amewapongeza vijana hao kwa kuwasilisha mapendekezo yao na hatua za kutatua changamoto zinazowakabili zikiwemo; changamoto za Watoto wenye mahitaji maalum, kuzuia mimba za utotoni, usafiri kwa wanafunzi na changamoto nyingine wanazowakabili vijana balehe kwa jumla na kuahidi kuhakisha changamoto hizo zitataftiwa ufumbuzi na Serikali.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku amesema kipaumbele kitachochukuliwa hatua kwa haraka katika mapendekezo yaliyotolewa ni kuimarisha uratibu wa Ajenda ya Vijana Balehe (NAIA) katika ngazi za Mikoa na halmashauri.
“Inabidi mikutano kama hii isifanyike tu katika ngazi ya taifa bali ifanyike pia katika ngazi za mikoa na halmashauri na hii itatusaidia kuwafikia vijana wengi kama si wote na kuweza kutatua changamoto zinazowakabili na hatimaye kufikia maadhimio ya ajenda hii” amesema Kitiku.
Vilevile, Mwakilishi wa vijana balehe anaewakilisha vijana wenye mahitaji maalum Latasonia Paul ameiomba serikali kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa elimu kwa vijana balehe hususani wenye mahitaji maalum kwa kujenga shule moja ya watoto wenye mahitaji maalum katika kila kanda nchini ili waweze kufikia ndoto zao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa wadau wa maendeleo kutoka Shirika la Nutrion International, Laureta Lucas ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya na kuiomba kuendelea kuwaongoza kuhakikisha afua za vijana balehe zinatekelezwa nchini kote.
0 Comments