Na Asha Mwakyonde, DODOMA
DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Kinywa na Meno kutoka Hospitali Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa, Dk.Alex Kimambo ameeleza kwamba lishe duni inachangia magonjwa ya meno kwa kuwa upungufu wa virutubisho muhimu kama calcium, vitamini D, na fluoride unaweza kudhoofisha meno na fizi.
Pia amesema watu wenye ugonjwa wa kisukari, hasa wale walio na kisukari kisichodhibitiwa, wanaweza kuwa na viwango vya juu vya sukari mdomoni, jambo ambalo linachochea bakteria kuzaliana na kusababisha magonjwa ya meno na fizi.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi, daktari huyo amesema kuwa lishe bora ni muhimu kwa afya ya meno.
Daktari huyo alieleza kuwa magonjwa ya kisukar iyanaweza kuongeza hatari ya magonjwa ya meno.
Amefafanua kwamba kukosa mate (Dry Mouth),kunasababisha mdomo kuwa na viwango vya chini vya mate ambavyo husaidia kutunza afya ya meno kwa kupunguza bakteria.
Daktari huyo ameeleza kuwa mate husaidia kusafisha mdomo na meno na kwamba hali hiyo inaweza kusababishwa na magonjwa, matumizi ya dawa, au umri mkubwa.
Ameongeza kuwa magonjwa ya meno yanaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, huku akisema mara nyingi magonjwa hayo huletwa na bakteria na tabia duni za usafi wa kinywa.
"Baadhi ya sababu kuu zinazochangia magonjwa ya meno,bakteria na Plaque,bakteria ni moja ya sababu kuu za magonjwa ya meno,"ameeleza daktari huyo.
Ameeleza kuwa bakteria hao huishi mdomoni, na kwenye plaques (mabaki ya vyakula ya muda mrefu kwenye meno) na husababisha asidi ambayo inaharibu enameli ya meno,tabaka la nje la meno.
"Plaque hii inapokaa kwenye meno kwa muda mrefu bila kusafishwa, inaweza kubadilika kuwa ugaga,tartari (calculus), ambayo ni vigumu kuiondoa kwa kusafisha meno tu," amesema.
Daktari Kimambo amefafanua kuwa Tartari hiyo husababisha ugonjwa wa fizi na kutoboka kwa meno huku akisema sukari na vyakula vyenye Asidi ni chakula cha bakteria mdomoni.
Ameongeza kuwa bakteria hutumia sukari kuunda asidi inayoharibu enamel ya meno na kwamba kula vyakula vyenye sukari nyingi kama pipi, keki, soda, na vinywaji vya nishati huongeza hatari ya kutoboka kwa meno.
Daktari huyo ameeleza kuwa vinywaji vyenye asidi kama soda na juisi za matunda vinaweza kuharibu enamel ya meno kwa sababu ya asidi inayozalishwa na vyakula hivyo.
Amesema upungufu wa madini ya Fluoride ni madini ambayo husaidia kuimarisha enamel ya meno na kuzuia kuoza.
Kimambo amefafanua kuwa upungufu wa fluoride, hasa kwenye maji ya kunywa au dawa za meno, unaweza kufanya meno kuwa dhaifu na kuwa hatarini kupata magonjwa ya meno.
"Kutosafisha meno vizuri kwa mswaki au mara kwa mara kuswaki meno mara mbili kwa siku ni njia muhimu ya kuzuia magonjwa ya meno, ikiwa huswaki meno vizuri au kwa wakati mzuri, plaque itajikusanya na kuwa chanzo cha bakteria wanaoharibu meno,"amesema.
Amesema kuwa tabia za Kunywa vinywaji vyenye sukari au Asidi mara kwa mara kunywa soda, juisi, au vinywaji vya kafeini kunatoa fursa kwa bakteria kuzalisha asidi ambayo inaharibu enamel ya meno.
Daktari huyo ameeleza kuwa kunywa vinywaji vyenye asidi mara kwa mara kunaweza kupunguza nguvu ya enamel ya meno na kuongeza hatari ya kuoza kwa meno.
Akizungumzia mabadiliko ya homoni wakati wa ujauzito, balehe, na menopause amesema yanaweza kuathiri afya ya meno na fizi, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya meno.
"Kwa mfano, wanawake wanapokuwa na mimba, wanaweza kuwa na tatizo la gingivitis (magonjwa ya fizi), ambalo linachangia kuoza kwa meno," amesema Daktari huyo.
Aidha ameeleza kuwa uvutaji sigara ni moja ya sababu za magonjwa ya fizi na meno ambapo inaharibu afya ya fizi na kuchangia kuzalishwa kwa bakteria wanaoharibu meno na fizi.
0 Comments