Na Asha Mwakyonde, Dodoma
HOSPIITALI Benjamin Mkapa (BMH), imafanikiwa kuweka vipandikizi maalumu kwenye uume (Penile Implantation),kwa wanaume 5 ambao walikuwa changamoto za upungufu wa nguvu za kiume.
BMH ni Hospitali ya kwanza kutoa huduma hiyo ya vipandkizi uume hapa nchini katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma Machi 4,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Profesa Abel Makubi wakati akizungumzia mafanikio na mwelekeo wa BMH katika kuelekea miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk.Samia.
Akizungumzia mafanikio na uboreshaji na kuongeza huduma za Tiba za Kibingwa na Ubingwa wa Juu ameeleza kuwa BMH kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), zimekuwa zikitoa na kupanua huduma za tiba za kibingwa na Ubingwa wa juu wa Tiba na upasuaji kwa Wananchi mbalimbali wapatao million 14 kutoka mikoa zaidi ya 7 ya Tanzania.
Prof. Makubi amesema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita chini Rais Dk. Samia Hospitali ya BMH, ikitumia falsafa ya 4Rs (Reforms, Rebuilding, Reconciliation na Resilience,), imepanua huduma za kibingwa kutoka 14 hadi 20 na huduma za ubingwa wa juu kutoka 7 hadi 16.
Amefafanua kuwa huduma hizo za ubingwa wa juu ni pamoja na Upandikizaji figo (kidney transplant), upandikizaji uloto (Bone marrow transplant), upasuaji wa mishipa ya damu (cardiovascular surgery), upasuaji wa Moyo kwa kufungua kifua (cardiothoracic surgery), uvunjaji wa mawe kwenye mfumo wa mkojo kwa kutumia mawimbi (external shock wave and laser lithotripsy) na upandikizaji uume(penile implantation).
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema huduma nyingine ni upasuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu (neuro and spine surgery), upasuaji wa uti wa mgongo (spine surgery), kubadilisha nyonga na magoti (hip and knee replacement), upasuaji wa matundu madogo (laparoscopic and endoscopic surgery), matibabu ya mfumo wa chakula (gastroenterology), matibabu ya magonjwa ya figo (Nephrology), uchujaji damu (Dialysis), matibabu ya magonjwa ya Moyo (cardiology), uchunguzi na matibabu ya mishipa ya moyo kupitia maabara ya uchunguzi (catheterization laboratory).
"Uchunguzi na matibabu ya kiradiolojia (interventional radiology),Tiba ya Magonjwa ya Hormone na kisukari(Endocrinology and Diabeteology) na Huduma za upandikizaji Mimba (IVF),Kuimarishwa na kuboreshwa kwa huduma za upandikizaji figo," amesema.
Ameongeza kuwa BMH imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 25 kati ya 50 kwa ndani ya miaka minne kwa gharama ya milioni 875, kati ya hao wagonjwa 10 wamelipiwa matibabu hayo kupitia mfuko maalum wa Rais Dk. Samia kwa kiasi cha shilingi milioni 350.
Prof. Makubi ameeleza kuwa endapo wagonjwa hao wangekwenda kufanyiwa huduma hiyo nje ya nchi Serikali ingetumia Shilingi bilioni 1.875, hivyo kiasi cha Shilingi bilioni 1 kimeokolewa.
0 Comments