Na Asha Mwakyonde
MBUNIFU wa mradi wa kifaa cha kufundishia Mfumo wa Jua, Sayansi ya Anga na Muundo wa Atomu Ernest Maranya ambaye ni mhitimu kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), amewaomba wadau mbalimbali ambao wapo tayari kwa ajili ya kufanya uwekezaji kwenye mradi huo ili Kifaa hicho kiingie katika uwekezaji mkubwa wa kibiashara.
Kifaa hicho cha kufundishia kimeizinishwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na kurasimishwa kuwa mtaala wa kufundishia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Akizungumza leo Juni 30,2025 katika banda la VETA katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, ‘Saba Saba’ ameeleza mtaala uliotolewa ni mpana na kwamba ni wa nchi nzima huku akisema anahitaji watu ambao wanaweza kufanya kazi kwa kushirikiana kwa lengo la kuzalisha vifaa vingi zaidi na kusambazwa shuleni.
Maranya amesema kuwa amekuwa na bunifu mbalimbali ambazo zinaisaidia jamii katika kukabiliana na changamoto kwenye maeneo wanaoyoishi.
Mbunifu huyo ameeleza kuwa kwa sasa anafanya kazi zake kwa kujitegemea na kwamba amejiari kupitia fani hiyo.
"Nimetoa mtaala wa kufundishia shule ya msingi na sekondari tangu mwaka 2023 ambapo hadi sasa Kifaa hiki kimeanza kuzifikia shule hizo zaidi ya shule 10 katika majarida ya awali.
Amefafanua kuwa bado wanaendelea na mchakato zaidi kwa ajili ya kufanya uzalishaji ili waweze kupata vifaa vingi vya kukidhi mahitaji katika shule hizo.
Mbunifu huyo amesema uhitaji ni mkubwa kuliko uwezo wake wa kuzalisha vifaa hivyo.
Aidha ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na wizara ya elimu na Tume Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kwa ushirikiano wa muda mrefu ambao wameendelea kumpatia.
Mbunifu huyo ameeleza kuwa anaendelea kupatiwa ushirikiano ambapo hadi sasa ushirikiano huo wa kuangalia namna ya kufanya uzalishaji mkubwa.
0 Comments