MWENEZI WA CHAUMMA ATIMKIA CCM


 Na Mwandishi wetu 

KATIBU wa zamani wa Uenezi wa Chama cha Ukombozi cha Umma (CHAUMMA) Mkoa wa Geita, Michael Godwin, ametangaza kujiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Geita, mara baada ya kukaribishwa rasmi ndani ya CCM na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, Godwin amesema uamuzi wake umetokana na kuridhishwa na kasi ya maendeleo yanayotekelezwa na Serikali ya CCM.

Amesema amevutiwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, huduma za afya na ustawi wa watumishi wa umma, akieleza kuwa ushahidi wa mafanikio hayo unaonekana wazi kwa wananchi.

“Geita imekuwa mfano wa mabadiliko chanya kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali, hatua ambayo imepunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwa muda mrefu,” amesema Godwin.

Akizungumza mara baada ya kumpokea Godwin, Kihongosi amesema CCM ni kimbilio la wengi na kusisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kupokea wanachama wapya na kufanya usajili kwa kasi kubwa.

“CCM tunafanya usajili kama timu ya Simba; wengine huko watasema amenunuliwa, ila wao wakipata hawajasema wamenunua,” amesema Kihongosi.


Post a Comment

0 Comments

SIASA NI HESABU, MTAJI WA WANACHAMA WAIBEBA CCM