Na Mwandishi wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kufurahishwa na kufunguliwa kwa shughuli za kisiasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha demokrasia ya ushindani wa kisiasa nchini.
CCM imesema sasa ni wakati wa vyama hivyo kukutana katika ulingoni na kushindana kwa hoja kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumza mkoani Geita, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amesema uamuzi huo unatoa nafasi pana kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa uwazi zaidi na kuongeza ushindani wenye tija katika siasa za Tanzania.
“Na kwa nini sisi kama chama tumefurahi? Tunatamani sasa tuingie ulingoni… nimesikia watazunguka nchi nzima, tutakutana huko, sisi tunawasubiri kwa hamu kubwa."
Kihongosi amesema ushindani wa kisiasa unapaswa kuwa wa kistaarabu na wenye tija kwa taifa.
Amesisitiza kuwa CCM iko tayari kushindana kutokana na mtandao wake mkubwa wa wanachama nchi nzima.


0 Comments