TUME YA MADINI YAAHIDI KUONGEZA FURSA ZA UWEKEZAJI KWA VIJANA


 Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

TUME ya Madini kupitia Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana na kundi la vijana katika kuhakikisha rasilimali iliyopo inawanufaisha ipasavyo pamoja na Taifa kwa ujumla ambapo dhamira ya dhati ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha rasilimali hiyo inawanufaisha Watanzania hususan vijana.

Hayo yamesemwa leo Machi 16,2026 jijini hapa na Mkurugenzi wa ukaguzi wa migodi na mazingira Mhandisi Hamisi Kamando kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo,

wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutangaza miradi ya maendeleo na fursa za vijana kwa mwaka 2025/2026, amesema ni jukumu la Wizara ya Madini kupitia Tume hiyo kuhakikisha rasilimali inasimamiwa na kutekeleza dhamira ya Rais kwa kushirikiana na vijana.

"Tukirejea katika hotuba Rais Dk. Samia ya ufunguzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa Novemba14, 2025 alisisitiza juu ya kuhakikisha rasilimali madini inawanufaisha vijana wasasa pamoja na vizazi vijavyo.Hivyo ni jukumu la Wizara yetu kupitia Tume ya Madini kuhakikisha rasilimali hii inasimamiwa na kutekeleza dhamira ya Rais kwa kushirikiana na vijana," amesema.

Mhandisi Kamando ameeleza kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Tume ya Madini inatarajia kuyatilia mkazo katika kipindi cha mwaka 2026/2027 kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa kundi la vijana ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi kupitia zabuni zitakazotangazwa.

"Nitoe rai kwa vijana kuangalia fursa zitakazokuwepo katika utekelezaji wa miradi hii uendelezaji wa minada na maonesho ya ndani ya madini ya vito pamoja na kutenga maeneo zaidi kwa vijana kila mkoa kulingana na aina ya madini yaliyopo kwenye mkoa husika," amesema Mhandisi Kamando.

Ameongeza kuwa Tume hiyo itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia pamoja na ujuzi wa utumiaji vifaa vya kisasa katika utafutaji na uchimbaji wa madini; na kushirikiana na Taasisi za kifedha mfano benki katika kuangalia namna bora ya upatikanaji wa mitaji kwa vijana ili kuweza kuhimili uwekezaji katika sekta ya madini.

Mhandisi Kamando ameeleza kuwa Tume hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa STAMICO na kituo cha Jemolojia cha Tanzania, imeendelea kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wachimbaji hasa vijana katika eneo la uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani pamoja na biashara ya Madini. 

Aidha amefafanua kuwa Tume ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini (Upskills Program) ilitoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo 579 wanaohusika na umiliki wa leseni, maduara, mialo pamoja na wafanyabiashara wa madini katika Mikoa ya Kimadini ya Geita, Mbogwe na Chunya. 

Lengo kuu la kuundwa kwa Tume ya Madini ni kuboresha usimamizi na udhibiti wa uzalishaji na biashara ya madini kwa kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazoongoza shughuli za madini zinafuatwa ipasavyo ili kuongeza Pato la Taifa.

Pia Tume hiyo ikiwa ni miongoni mwa taasisi zinazotekeleza miongozo mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM ya Mwaka 2025 inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia imeendelea kuandaa na kuweka mazingira wezeshi juu ya ushirikishwaji wa vijana katika fursa zinazotokana na shughuli za Madini nchini. 

Post a Comment

0 Comments

TUME YA MADINI YAAHIDI KUONGEZA FURSA ZA UWEKEZAJI KWA VIJANA