Tanga
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Juma Homera amepongeza maendeleo makubwa ya mifumo ya kidigitali ya ufundishaji katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama kilichopo Lushoto mkoani Tanga Region.
Akizungumza wakati wa ziara yake chuoni hapo Machi 24, 2026, Waziri Homera amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na chuo hicho katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kufundishia majaji, mahakimu pamoja na watumishi wengine wa mhimili wa mahakama.
Amesisitiza kuwa mifumo hiyo ya kidigitali imeongeza ufanisi, uwazi na ubora wa mafunzo yanayotolewa, hali inayochangia moja kwa moja kuimarika kwa utoaji wa haki nchini.
“Kwa kweli nimefurahishwa sana na kiwango cha matumizi ya teknolojia hapa chuoni. Mifumo ya kidigitali iliyowekwa imeboresha kwa kiasi kikubwa mbinu za ufundishaji na ujifunzaji. Hii ni hatua muhimu katika kujenga mahakama yenye weledi na ufanisi wa hali ya juu,” amesema Mhe. Homera.
Aidha, ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kinakuwa kituo bora cha umahiri si tu nchini bali pia barani Afrika, kwa kuzalisha wataalamu mahiri watakaohudumia sekta ya sheria kwa ufanisi mkubwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya chuo, Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, alieleza kuwa taasisi hiyo imeendelea kuzalisha wataalamu wenye weledi kwa kuwapatia nyenzo muhimu za uendeshaji wa mashauri mahakamani.
Dkt. Kihwelo amzeonhaeza kuwa kupitia mfumo wa kidigitali wa mafunzo kwa njia ya mtandao unaojulikana kama *IJA e-LMS*, chuo kimefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi na kupanua wigo wa upatikanaji wa mafunzo kwa wadau mbalimbali wa sekta ya sheria.
Mafanikio hayo yanaakisi juhudi za Serikali katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwenye sekta ya Sheria nchini.








0 Comments