Dar es Salaam
TUME ya Ushindani (FCC) leo Machi 26, 2026 imetoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mnazi Mmoja iliyopo jijini Dar es Salaam kuhusu kumlinda mlaji, ikiwemo haki na wajibu wa mlaji pamoja na madhara ya matumizi ya bidhaa bandia katika jamii.
Elimu hiyo imelenga kuwajengea wanafunzi uelewa wa awali kuhusu umuhimu wa kuchagua na kutumia bidhaa zilizo salama, huku ikisisitiza kuwa walaji wana nafasi kubwa katika kulinda afya zao na za wengine.
Akizungumza na wanafunzi hao,Afisa Mlinda Mlaji kutoka FCC Bi.Techla Kitosi,amesisitiza umuhimu wa watumiaji kuwa na uelewa wa haki zao wanaponunua bidhaa au huduma. Ameeleza kuwa mlaji ana haki ya kupata bidhaa bora, salama na zenye ubora unaokubalika.
Aidha ameonya dhidi ya ununuzi wa bidhaa bandia ambazo zinaweza kuhatarisha afya na usalama wa mtumiaji.
“Ni muhimu sana kwa kila mmoja wenu kujifunza kutambua bidhaa halisi na bandia. Msikubali kudanganywa na bei ndogo bila kuangalia ubora wa bidhaa,” amesema Bi.Kitosi
Kwa upande wake, Afisa Mlinda Mlaji Mwandamizi, Magdalena Hall, ameeleza wajibu wa mlaji kuwa ni pamoja na kusoma maelekezo ya matumizi ya bidhaa, kuhifadhi stakabadhi za manunuzi na kutoa taarifa pale wanapokutana na bidhaa zisizo na viwango.
Hata hivyo Bi.Hall ,amewahamasisha wanafunzi kuwa mabalozi wa ulinzi wa mlaji katika jamii zao kwa kutoa elimu kwa familia na marafiki kuhusu madhara ya bidhaa bandia.
Wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kupewa majibu ya kina, jambo lililosaidia kuongeza uelewa wao kuhusu masuala ya ulinzi wa mlaji.
Elimu hiyo ni sehemu ya jitihada za Tume ya Ushindani kuendelea kutoa elimu kwa umma, hususan vijana, ili kujenga jamii yenye uelewa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa na huduma.
Mafunzo hayo ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani, tukio linaloadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu haki za walaji duniani kote.







0 Comments