Na Asha Mwakyonde, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA),ilianzisha zoezi la kusanifu na kujenga mfumo mpya wa ununuzi wa Umma wa National e-Procurement System of Tanzania NeST ikiwa ni mahitaji mapya ya Teknolojia pamoja na maelekezo ya Serikali ya kuimarisha eneo la ununuzi wa Umma nchini hususan katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Pia kwa kuhakikisha mfumo huo unaeleweka na unatumika kwa ufasaha, PPRA imejipanga na imeanza kutoa mafunzo kwa Taasisi Nunuzi na Wazabuni kote nchini na itashirikiana na Vyuo vya Elimu ya Juu katika kuhakikisha mafunzo hayo ya NeST yanawafikia watumiaji wote.
Akizungumza jijini Dodoma Juni 23,2023 na Waandishi wa Habari kuhusu kuanza kutumika kwa mfumo huo Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA Dk. Leonada Mwagike amesema kifungu Namba 9 (1)(k) cha sheria ya Ununuzi wa Umma, sura 410 kimeipa mamlaka hiyo jukumu la kubaini, kujenga na kusimamia mifumo ya kielektroni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za ununuzi huo nchini.
Mwenyekiti huyo amesema sababu kubwa iliyosababisha ujenzi wa mfumo huo wa NeST ni hitaji la kuhakikisha ununuzi wa Umma unazingatia misingi mikuu ya kimataifa katika ununuzi ambayo ni uwazi( Transparency), Usimamizi mzuri wa fedha za Umma, kuzuia mwenendo mbaya, Ukidhi na ufuatiliaji, uwajibikaji na uthibiti .
Akizungumzia matarajio ya mfumo huo ameeleza kuwa unatarajiwa kutatua changamoto kadhaa za kiufundi, kukidhi mahitaji ya serikali katika sekta ya ununuzi na kwamba mfumo wa NeST ulianza rasmi Julai 18, 2022 na hadi kufikia Julai 2023 moduli muhimu kwa ajili ya kuruhusu mfumo kuanza kutumika zimeshakamilika.
"Napenda kuuarifu Umma wa Watanzania kuwa kuanzia Julai 1, mwaka huu mfumo wa NeST utaanza kutumika rasmi katika michakato ya Ununuzi katika baadhi ya taasisi za Umma ambazo tayari zimeshapatiwa mafunzo," amesema.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa mfumo huo utatumika katika hatua zote za michakato ya Ununuzi kuanzia utangazaji wa zabuni hadi utoaji wa tuzo za zabuni hizo ambapo wataanza na Taasisi Nunuzi 101 katika awamu ya kwanza ambayo ni Julai 1, na zilizobaki zitaanza kutumia mfumo wa NeST Octoba 1 mwaka huu.
Akizungumzia vyuo vilivyoingia katika mfumo huo Mwenyekiti huyo amesema hadi sasa vyuo sita vimeshaingia katika makubaliano ya ufundishaji wa mfumo huo ambavyo ni Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA),Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya(MUST), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo cha Usimamizi wa fedha (IMF).
0 Comments