WAZAZI BAHI WATAKIWA KUACHA TABIA YA KUWAFICHA WATOTO WENYE ULEMAVU NDANI


 Dodoma

WAZAZI wenye watoto walemavu wametakiwa kuwapeleka watoto wao shule ili waweze kupata elimu kama watoto wengine na si kuwaficha nyumbani.

Wito huo umetolewa Juni 23, 2023 wilayani Bahi mkoani Dodoma na Mratibu wa Mradi wa Elimu Jumuishi Janey Mgidange wakati akiongea na wazazi hao wilayani humo, ambapo amesema kitendo cha kuwaficha nyumbani kinawanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.

“Wazazi tujitahidi katika hili. Langu kubwa na la msingi wazazi mhakikishe mtoto mwenye ulemavu anaenda shule. Ni wajibu wako kwa sababu umemleta mwenyewe, kwa hiyo unatakiwa ufuate Sheria ya Tanzania. Inasema mtoto anapofikisha umri wa miaka minne aende shule haijarishi ni mlemavu ama si mlemavu.” amesema Janey.

“Kuna mtu mwingine anasema sasa yule kiziwi anawezaje kwenda shule. Ulimpeleka shule ukaambiwa kwamba hakuna anayemuweza? Na kama ulimpeleka shule njoo uniambie ni wapi. Au kama haoni ulimpeleka shule wakasema sisi hatuwezi kumfundisha? Na kama ulimpeleka huyo mtoto njoo umuone hata Mtendaji wa Kata atatuambia  ni shule gani na ni mwalimu nani ambaye amemkataa huyo mtoto.” ameongeza Janey.

Diwani wa Kata ya Bahi wilayani humo Augustino Ndonu amesema baadhi ya watu wamekuwa na dhana ya kwamba mtoto anapozaliwa na ulemavu hapaswi kusoma jambo ambalo si kweli.

“Hivi mtoto wako mwenye ulemavu ndani ukimfungia ndani utakuwa umemfanyia ukatili au unampenda? Bila shaka unamchukia. Na haya mambo yanafanyika hapa, wazazi mnachukua hatua gani?” amehoji diwani huyo.

Katibu wa wazazi wenye watoto walemavu Rajab Mohamed wilayani humo amesema, wapo baadhi ya wazazi ambao wameshindwa kukubaliana na hali ya watoto wao kuwa ni walemavu, hali ambayo imepelekea kuanza kuwabagua wao wenyewe.

“Kutokukubali kunamfanya mzazi mwenyewe kumnyanyapaa mtoto. Hata wakati ambao ameweka chakula anamuwekea mlemavu peke yake na hawa wengine peke yao.” amesema Rajab.

Naye Maria Emanuel mzazi mwenye mtoto mlemavu,  ametumia hadhara hiyo kuwaelimisha wazazi kujua umuhimu wa kuwapenda na kuwathamini watoto wenye ulemavu na si kuwabagua.

“ Kina mama wenzangu mimi ni mzazi kama wengine nina mtoto mlemavu. Mtoto wangu sikutaka kumuweka ndani nilimuweka nje akaenda shule . Nawaomba wazazi hawa watoto ni sadaka kwa mwenyezi Mungu tusiwafiche. “ amesema Maria.

Ingawa Malengo ya Maendeleo Endelevu yanahimiza kuwa hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyumba, utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF unaonesha kuwa kati ya watoto milioni 240 wenye ulemavu duniani, nusu hawajawahi kuhudhuria shule.

Utafiti huo pia unaonesha, takriban theluthi moja hawapati chakula bora na cha kutosha na pia watoto wenye ulemavu wanawakilishwa kwa njia isiyo sawa na wengi wao wanaacha nyuma.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI