WATAALAM WA MAENDELEO WASHAURIWA KWENDA VIJIJINI KUTOA ELIMU YA SAYANSI YA MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA WATOTO


Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MAAFISA wa Maendeleo  wa mikoa pamoja na wadau wametakiwa kutumia ipasavyo elimu ya mafunzo ya Kitaifa ya Sayansi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto waliopatiwa katika maeneo yao ya kazi na kuhakikisha jamii inapata elimu hiyo ya malezi na Makuzi.

Pia maafisa, wataalam hao wametakiwa kuwa mabalozi katika mikoa wanayotoka hadi Vijijini ambako ndio kwenye shida wasio ona kwenye vyombo vya habari kwenda kutoa elimu hiyo.

Akizungumza jijini Dodoma Juni 26, 2023,Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaid Ali Khamis wakati akifungua mafunzo hayo ya siku sita, ameeleza kuwa wizara inatambua fursa hiyo ni ya kipekee ya kuongeza ujuzi na malezi ya watoto kwa wataalam hao.

Amesema  awali wataalam 180 wa maendeleo kutoka mikoa 10 walipatiwa mafunzo hayo  na kwamba hadi kufikia Disemba Wataalam hao  zaidi ya 200 watakuwa wamepatiwa mafunzo Kitaifa ya  Sayansi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto.


"Kundi la wataalam lililopo hapa ni muhimu katika kuongeza uwezo ili kuimarisha programu hii ya mafunzo ya Kitaifa ya Sayansi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto, natambua umuhimi wa Chuo cha Aga Khan kwa kuwezesha mafunzo haya," amesema.

Ameongeza kuwa baada ya mafunzo hayo  wanatarajia kuongeza idadi kubwa ya wataalam hao huku akisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anasisitiza elimu hiyo kwa kuwa ni mama.

"Tuendelee kumuunga mkono Rais Dk.Samia kwa kipindi cha miaka miwili amefanya mambo ya maendeleo katika Taifa letu, zingatieni mafunzo haya ili lengo la mafunzo ya malezi, makuzi ya awali ya mtoto yaweze kutimia, " ameeleza.


Awali Naibu katibu Mkuu  kutoka  Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Wakili Amon Mpanju amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza na kuendeleza ujuzi wa wataalam hao.

Ameongeza kuwa programu ya mafunzo hayo imezinduliwa katika mikoa 10 na kwamba washiriki 180 wametoka katika hiyo.

"Hadi kufikia Disemba mwaka huu  mikoa 26 itakuwa imezindua programu hii na jumla tutakuwa na wahitimu wengi zaidi ikijumuishwa wahitimu kupatiwa vyeti vya kimataifa," amesema.

Naye Afisa Maendeleo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa ShinyangaTedson Ngwale ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo akitoa neno la shukurani amesema Taifa lolote  duniani linawekeza kwenye watu ili liweze kupata maendeleo.

"Rais aliona kwa jicho la mbali akatuwekea wizara hii, tunaahidi kuitenda haki kupitia mafunzo haya amabyo ni muhimu kwa kwetu sisi na jamii kwa ujumla," amesema Ngwale.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI