KITOLINA KIPPA ATOA SOMO LA UTHUBUTU KWA WANAWAKE KATIKA BIASHARA


📍wanawake wajiamini na kuthubutu kufikia mafanikio ya kiuchumi

Na Asha Mwakyonde,DODOMA 

SIKU ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 8, ikiwa ni siku maalum ya kutambua mchango na juhudi za wanawake katika kujenga jamii bora. 

Kupitia maadhimisho haya, jamii hukumbushwa umuhimu wa kuendelea kupigania usawa wa kijinsia, kuwainua wanawake kiuchumi na kijamii pamoja na kuthamini nafasi yao katika maendeleo ya dunia.

Maadhimisho haya huchochea wanawake waliofanikiwa katika sekta mbalimbali kueendelea kutoa hamasa kwa wenzao kujitambua, kujenga ujasiri na kujikwamua kiuchumi. 

Miongoni mwao ni Mkurugenzi Mtendaji na mfanyabiashara anayemiliki hoteli ya Four Point pamoja na kumbi za sherehe na za mikutano jijini Dodoma, Kitolina Kippa, hatua inayodhihirisha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kufikia mafanikio wanapothubutu na kuwa na malengo thabiti.

Kippa anasema wanawake wa sasa wanapaswa kubadilika na kujenga misingi ya kujitegemea kiuchumi tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo wengi walitegemea kipato cha wanaume wao.

“Wanawake wa sasa tunatakiwa kujitambua. Wanawake wa zamani walikuwa wanawategemea wanaume wao, lakini sasa hivi iwe umeolewa au hujaolewa ni muhimu kuwa na uchumi wako mwenyewe,” anasema.

Anasema Mungu hakuwafanya wanawake kuwa viumbe dhaifu bali tofauti iliyopo ni ya jinsia tu, hivyo mwanamke ana uwezo wa kufanya chochote kinachoweza kufanywa na mwanaume.

Mkurugenzi Mkuu huyo anaeleza kuwa jambo muhimu kwa mwanamke ni kuwa na malengo ya kujikwamua kiuchumi, kuyapangilia vizuri na kuyatekeleza kwa vitendo ili kufikia mafanikio.

Kwa mujibu wa Kippa, hata wanaume wengi wanafanikiwa kutokana na mchango wa wanawake kwa kuwa wanawake mara nyingi huwa washauri wakuu wa waume zao.

“Mwanaume anayefanikiwa mara nyingi nyuma yake kuna ushauri mzuri wa mwanamke wake,” anasema.

Anasema katika dunia ya sasa wanawake wanapaswa kutambua kuwa wana nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla kwa kuongeza thamani katika shughuli wanazofanya.

Kippa anaamini kuwa mwanamke ana uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa endapo ataacha kujiona mnyonge na badala yake akajiamini.

Anaeleza kuwa siku hiyo ni muhimu kwa wanawake kwa sababu inawakumbusha kujivunia uwanawake wao na kutambua kuwa wao ni nguzo muhimu katika ujenzi wa Taifa kuanzia ngazi ya familia hadi jamii kwa ujumla.

HOFU YA KUTHUBUTU

Kippa anasema moja ya changamoto inayowarudisha nyuma wanawake wengi ni hofu ya kujaribu kufanya mambo mapya.

Anashauri wanawake kuanza na kile wanachoweza kufanya hata kama ni biashara ndogo kama kupika maandazi, ilimradi wawe na ujasiri, kujiamini na kufanya kazi kwa bidii.

“Tuache woga wa kufikiria hatutaweza. Jaribu kwanza ndipo useme umeweza au umeshindwa. Usijikatishe tamaa kabla hata hujaanza,” anasisitiza.

USHAURI KWA SERIKALI

Kuhusu mchango wa serikali, Kippa anasema ni muhimu kuweka mazingira rafiki kwa wanawake wengi ambao ni wajasiriamali wadogo ili waweze kukuza biashara zao.

Anashauri kuwepo kwa masoko bora ya bidhaa, pamoja na kuwezesha wanawake kupata mitaji na mikopo itakayowasaidia kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Aidha, anaiomba serikali kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali mara kwa mara ili kuwajengea wanawake uelewa na uwezo wa kuendesha biashara zao kwa ufanisi.

NDOTO ZA BAADAYE

Kippa anasema licha ya mafanikio aliyoyapata hadi sasa, bado ana ndoto kubwa zaidi za kupanua uwekezaji wake.

Anaeleza kuwa tayari ameongeza vyumba 17 katika hoteli yake na anaendelea na ujenzi ili kuongeza vyumba zaidi na kuboresha huduma anazozitoa.

“Bado nina ndoto ya kufika juu zaidi. Natamani kuwa na uwekezaji mkubwa zaidi utakaoniwezesha kuendesha maisha yangu na kutoa ajira kwa wengine,” anasema.

UJUMBE KWA WANAWAKE NA VIJANA 

Kippa anawahimiza wanawake na vijana kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa ili kupata maarifa, mbinu na ujuzi wa kufanikisha shughuli zao za kiuchumi.

Anasema vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu hukimbilia kutafuta ajira serikalini badala ya kujiajiri.

Ni vema vijana kubadili mtazamo huo na kujikita katika ujasiriamali ili baadaye waweze kuwaajiri wenzao.

AJIRA KWA WANAWAKE

Katika kuonesha dhamira ya kuwainua wanawake, Kippa anasema katika hoteli yake ameajiri vijana 10 ambapo wanawake ni sita na wanaume ni wanne.

Pia anasema kuna wanawake wengine wanaofika katika hoteli hiyo kujifunza na kupata uzoefu wa biashara ili waweze kujikwamua kiuchumi.

KUKATISHWA TAMAA

Kippa anasema safari yake ya mafanikio haikuwa rahisi kwani alikumbana na changamoto nyingi ikiwemo kukatishwa tamaa na baadhi ya watu, wakiwemo wanawake wenzake.

Anasema wakati anaanza ujenzi wa hoteli hiyo, baadhi ya watu walimwambia anapoteza fedha zake na kwamba hatoweza kumaliza mradi huo.

“Waliniambia fedha zitaishia kwenye ujenzi huu na sitoweza kuendelea. Lakini nilijiamini na kuendelea kupambana hadi nilipofikia hapa,” anasema.

Anasisitiza kuwa badala ya kukatishana tamaa, wanawake wanapaswa kupeana moyo na kusaidiana ili kufikia mafanikio makubwa zaidi katika jamii.

Post a Comment

0 Comments

e-GA YATOA MSAADA KWA WATOTO WENYE UHITAJI