TMA YATOA UTABIRI: MVUA NA NGURUMO KUNYESHA MAENEO MBALIMBALI NCHINI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo, Februari 25, 2026, ikieleza kuwa maeneo mbalimbali nchini yanatarajiwa kuwa na mawingu, mvua na ngurumo za radi huku baadhi yakipata vipindi vifupi vya jua.

Kwa mujibu wa TMA, hali ya mawingu, mvua na ngurumo inatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, pamoja na Tabora, Kigoma na Katavi, na Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu.

Katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, kunatarajiwa mawingu, mvua na ngurumo katika maeneo machache sambamba na vipindi vifupi vya jua. Hali kama hiyo pia inatarajiwa katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam, pamoja na Mkoa wa Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia.

Kwa upande wa mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe, pamoja na Mtwara na Lindi, kutakuwa na mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.

ANGALIZO LA MVUA KUBWA 

TMA imetoa angalizo la vipindi vifupi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa katika maeneo machache ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro na Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

VIWANGO VYA JOTO 

Kwa mujibu wa takwimu za TMA, viwango vya juu vya joto leo vinatarajiwa kuwa nyuzi 31°C katika mji wa Tanga, 30°C Dar es Salaam na Zanzibar, huku Arusha ikitarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha 24°C. Dodoma inatarajiwa kufikia 27°C, Mwanza 26°C na Kigoma 27°C.

Kwa Nyanda za Juu Kusini, Mbeya inatarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha 22°C na Njombe 21°C, hali inayoashiria baridi kiasi katika maeneo hayo.

UPEPO NA HALI YA BAHARI 

Kwa ukanda wa pwani, upepo unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya kilomita 20 kwa saa; ukitokea mashariki kwa pwani ya kaskazini na kaskazini mashariki kwa pwani ya kusini. Hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi madogo.

MATARAJIO YA SIKU ZIJAZO 

Kwa mujibu wa TMA, matarajio ya siku ya Ijumaa, Februari 27, 2026, ni kuendelea kwa vipindi vya mvua katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Mamlaka hiyo imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua tahadhari stahiki hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua kubwa za muda mfupi.

Post a Comment

0 Comments

TMA YATOA UTABIRI: MVUA NA NGURUMO KUNYESHA MAENEO MBALIMBALI NCHINI