TAEC: MAANDALIZI YA UZALISHAJI WA UMEME WA NYUKLIA YAANZA KWA KUZINGATIA USALAMA


Na Asha Mwakyonde DAR ES SALAAM 

TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), imesema Serikali imeanza kuweka msingi wa utekelezaji wa mpango wa kuzalisha umeme wa nyuklia kwa kuimarisha mifumo ya kisheria, sera na taasisi, huku ikisisitiza kuwa kila hatua inayochukuliwa inalenga kuhakikisha usalama wa wananchi na mazingira kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Mradi wa kwanza wa uchimbaji wa urani unatarajiwa kuanza katika eneo la Mkuju, mkoani Ruvuma, huku tafiti zikiendelea katika maeneo mengine ili kubaini maeneo yenye akiba zaidi ya madini hayo.

Akizungumza leo Julai 5,2026 Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Kassim Mohammed, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF),maarufu Sabasaba,amesema Tanzania ipo katika hatua za maandalizi ya awali kabla ya kuanza rasmi utekelezaji wa mpango huo unaoongozwa na miongozo ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Amesema Serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi yatakayohakikisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia yanafanyika kwa usalama na kwa kuzingatia taratibu zote zinazotakiwa kimataifa.

"Tunajenga msingi imara utakaowezesha matumizi salama ya nishati ya nyuklia, ili nchi iweze kuingia katika uzalishaji wa umeme kwa kujiamini na bila kuhatarisha afya za wananchi au mazingira," amesema Prof. Najat.

Amefafanua kuwa TAEC tayari imewashirikisha wataalamu wa kimataifa kufanya tathmini ya kiwango cha utayari wa Tanzania, ambapo matokeo yake yataamua hatua inayofuata kuelekea utekelezaji wa mradi huo.

Kwa mujibu wa Prof. Najat, Serikali inalenga ndani ya kipindi cha takribani miaka saba kufikia hatua ya kuzalisha umeme wa nyuklia, ambao unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya kukuza uchumi, viwanda na shughuli nyingine za maendeleo.

Akizungumzia upatikanaji wa malighafi, ameeleza kuwa Tanzania ina akiba ya madini ya urani, ambayo ni malighafi muhimu katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia.

Hata hivyo, amebainisha kuwa urani huhitaji kuchakatwa kwa teknolojia maalumu kabla ya kutumika kuzalisha mafuta ya nyuklia.

Ameongeza katika hatua za mwanzo, urani itachimbwa nchini na kusafirishwa katika nchi zenye uwezo wa kuichakata, ikiwemo Urusi, kabla ya kurejeshwa nchini ikiwa tayari kwa matumizi ya kuzalisha umeme.

Aidha,amewataka wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu matumizi ya teknolojia ya nyuklia na kuondoa hofu zisizo na msingi, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa usalama, ufanisi na manufaa ya maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments

TAEC: MAANDALIZI YA UZALISHAJI WA UMEME WA NYUKLIA YAANZA KWA KUZINGATIA USALAMA