Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kampasi ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), kimesema kinaendelea kufanya tafiti za kuongeza thamani ya zao la ulanzi kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotumika katika sekta za afya, elimu, utafiti na nishati, hatua inayolenga kukuza uchumi na kuifanya kilimo cha ulanzi kuwa cha kibiashara zaidi.
Mhadhiri Mwandamizi kutoka MUCE, Dk. Lewis Mtashobya, amesema hakuna sababu ya kuendelea kuuza malighafi pekee wakati tafiti zimeonesha kuwa ulanzi unaweza kuzalisha bidhaa nyingi zenye thamani kubwa.
Amesema taasisi hiyo ilianza kufanya tafiti kuhusu ulanzi na imeendelea kuziendeleza, jambo lililowezesha kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo.
Kwa mujibu wa Dk. Mtashobya, miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa ni solvent, aina ya ethanoli inayotumika kama kiyeyusho katika maabara za shule, vyuo na taasisi za utafiti kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kisayansi.
Aidha, amesema wamefanikiwa kuzalisha spiriti ya tiba (medical spirit) inayotumika hospitalini kusafisha sehemu ya mwili kabla ya kutoa sindano ili kuzuia maambukizi.
Pia wamezalisha kimiminika maalumu cha kuhifadhia sampuli za viumbe hai, ambacho ni mbadala salama wa formalini, kemikali ambayo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu lakini ina madhara kwa afya ya binadamu.
Dk. Mtashobya amesema tafiti hizo pia zimewezesha uzalishaji wa ethanoli yenye viwango vya juu vya usafi, ambapo walianza na kiwango cha asilimia tano na sasa wamefikia asilimia 92.
Ameeleza kuwa ethanoli yenye usafi wa asilimia 80 hadi zaidi ya asilimia 90 hujulikana kama fuel grade ethanol na inaweza kutumika kuendesha mashine na magari.
Amesema matumizi ya nishati ya mimea (biofuel) yanaongezeka duniani kutokana na kuwa ni nishati safi isiyochangia kwa kiwango kikubwa utoaji wa gesi chafuzi zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuchangia katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.
Amesisitiza kuwa kuongeza thamani ya zao la ulanzi kupitia tafiti ni hatua muhimu ya kufungua fursa mpya za ajira, viwanda na kuongeza kipato cha wakulima pamoja na uchumi wa taifa.



0 Comments