BRELA YAWAVUTIA WAJASIRIAMALI KWA HUDUMA ZA HARAKA ZA KIDIJITALI SABASABA

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

HUDUMA za kidijitali zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) zimeendelea kuwavutia wafanyabiashara na wajasiriamali wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), huku wakieleza kuridhishwa na kasi ya utoaji wa huduma za usajili wa majina ya biashara, kampuni na leseni kupitia mfumo wa BRELA Online Services (BOS).

Mmoja wa wanufaika wa huduma hizo, Abdulher Misana, amesema ametembelea banda la BRELA kwa lengo la kusajili jina jipya la biashara kwa ajili ya kuanzisha shughuli nyingine za kibiashara, ambapo amehudumiwa na kukamilishiwa usajili wake kwa mafanikio.

"Leo nimekuja hapa kwenye banda la BRELA kwa sababu nataka kuongeza biashara nyingine katika sekta tofauti na ile niliyokuwa nayo awali," amesema Misana.

Akizungumzia mfumo mpya wa BRELA Online Services (BOS), amesema umeboreshwa na kuleta mabadiliko makubwa yanayorahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara.

"Kila jambo jema halikosi changamoto, lakini nina matumaini BRELA itaendelea kuboresha mfumo huu. Timu yao imejipanga vizuri katika kuwahudumia wafanyabiashara wanaotaka kufanya biashara zinazotambulika kisheria na serikali," amesema.

Misana amesema alitumia takribani saa moja na nusu kukamilisha usajili wake na kuwahimiza wafanyabiashara kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata taratibu za kisheria.

Naye David Mwandiki amesema alifika katika banda la BRELA kuomba leseni ya biashara na kufanikiwa kuipata kwa muda mfupi.

Amesema upatikanaji wa leseni kwa haraka utawasaidia wafanyabiashara kuepuka changamoto zinazotokana na kufanya biashara bila vibali vinavyotakiwa.

"Ninawakaribisha wafanyabiashara na wajasiriamali wenzangu kufika katika banda la BRELA ili wapate huduma za usajili wa biashara, leseni na alama za biashara, zitakazowawezesha kufanya biashara kihalali bila usumbufu kutoka kwa mamlaka husika," amesema.

Kwa upande wake, Suleiman Fupi amesema alifika katika banda la BRELA kwa ajili ya kusajili kampuni yake na kufanikiwa kupata usajili huo, jambo alilosema limetimiza azma yake ya kufanya biashara kwa mujibu wa sheria.

"Nashukuru huduma za BRELA ni nzuri. Ukishasajili kampuni yako unakuwa sehemu ya mfumo rasmi wa serikali na unatambulika kisheria. Hatupaswi kubaki nje ya mfumo, kwani kufanya hivyo kutasaidia kuendesha biashara zetu kwa uhalali," amesema.

Fupi amewahimiza wafanyabiashara na wajasiriamali ambao bado hawajasajili biashara zao kufika katika banda la BRELA ili wapate huduma na kujiunga na mfumo rasmi wa biashara nchini.

Post a Comment

0 Comments

GENEVA: NEST YATWAA TUZO, MIONGONI MWA MIFUMO 20 BORA YA SERIKALI DUNIANI