📍Kapinga aipongeza NIDA kwa kuchochea uchumi jumuishi na Dira ya Taifa 2050
Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Judith kapinga ameipongeza Kiwanda cha NIDA Textile Mills (T) Ltd,kuwa jitihada zake za kuungana mkono serikali katika kuimarisha uchumi jumuishi na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kapinga ameyasema hayo leo Julai 8,2026 alipotembelea banda la NIDA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), 'Sabasaba' amesema ameembelea banda la la kampuni hiyo inayozalisha kanga na nguo nyingine za pamba huku akisema ndio maana wanaendelea kuwasiaitiza watanzania kwamba fursa zipo nyingi za kujifunza na kupanua mawanda ya biashara.
"Leo nimefika tena kama mnavyofahamu maonesho haya yanaratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania · (TANTRADE ),chini ya Wizara yetu ya Viwanda na Biashara," amesema.
Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Mohamed Honello ameeleza kuwa NIDA inaendelea kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la pamba kwa kutekeleza uzalishaji wa nguo kuanzia kwa mkulima hadi bidhaa kumfikia mlaji, huku akiiomba serikali kuweka utaratibu utakaowezesha pamba nyingi zaidi kubaki na kuchakatwa nchini ili kukuza viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Amesema kampuni inanunua pamba kutoka kwa wakulima na kuipeleka kiwandani ambako huchakatwa kuwa nyuzi, hutengenezwa vitambaa, huchapishwa na kushonwa kabla ya kupelekwa moja kwa moja katika maduka ya kampuni kwa ajili ya kuuzwa.
Meneja huyo amesema mfumo huo wa uzalishaji unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukuza viwanda, kuongeza ajira, kupanua masoko ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Honello ameeleza kuwa Tanzania ina pamba ya kutosha kukidhi mahitaji ya ndani, lakini changamoto iliyopo ni ukusanyaji, ununuzi na usimamizi wa zao hilo.
Ameeleza kuwa viwanda vingi haviwezi kununua pamba yote inayozalishwa kwa wakati mmoja, hivyo kuna umuhimu wa Serikali kuweka mfumo utakaowezesha pamba nyingi zaidi kubaki nchini na kununuliwa na wazalishaji wa ndani badala ya kuuzwa nje.
Amefafanua kuwa hatua hiyo itasaidia viwanda kununua pamba kwa awamu hadi kukidhi mahitaji yao ya mwaka mzima, kupunguza utegemezi wa kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi na kuongeza matumizi ya pamba inayozalishwa nchini.
Aidha, amsema matumizi makubwa ya pamba ya ndani yatawanufaisha wakulima kwa kuwapatia soko la uhakika, kuongeza thamani ya mazao yao na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Hata hivyo, Honello amebainisha kuwa gharama za uzalishaji nchini bado ni kubwa ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine, hali inayopunguza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini katika soko la ndani na nje ya nchi.
Ameitaka Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uzalishaji ili kupunguza gharama za uendeshaji wa viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko mbalimbali.
Akizungumzia suala la ajira, amesema kampuni ina ajiri wafanyakazi wa kudumu kati ya 1,500 na 2,000 kulingana na kiwango cha uzalishaji wa pamba.
Honello ameongeza kuwa wakati wa msimu wa mavuno ya pamba, kampuni huajiri wafanyakazi wengi zaidi wa muda kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji, hatua inayochangia kuongeza ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.



0 Comments