TUTUBA: BODI YA BIMA YA AMANA, NGAO YA USALAMA WA FEDHA ZA WANANCHI

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM 

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, amewahakikishia wananchi kuwa fedha wanazoweka katika benki na taasisi rasmi za kifedha ziko salama kutokana na ulinzi unaotolewa na Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board), akiwahimiza kuachana na tabia ya kuhifadhi fedha majumbani.

Hayo alisema leo Julai 10, 2026 alipotembelea banda la Bodi hiyo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF)" Sabasaba Tutuba amesema Bodi ya Bima ya Amana ilianzishwa mahsusi kulinda amana za wateja katika taasisi za fedha, hivyo kuwapa uhakika wananchi kwamba fedha zao zitaendelea kuwa salama hata endapo benki au taasisi ya kifedha itakumbwa na changamoto, ikiwemo kufilisika, kwa mujibu wa sheria.

Ameeleza kuwa fedha zinazowekwa benki huendelea kutumika katika shughuli mbalimbali za kifedha, lakini kila mweka amana hubaki na haki ya fedha zake ambazo hutambuliwa na kulindwa kupitia mfumo rasmi wa bima ya amana.

Kutokana na hali hiyo, Gavana huyo amewataka wananchi kuendelea kuziamini taasisi rasmi za kifedha kwa kuweka fedha zao benki badala ya kuzihifadhi majumbani, akisema hatua hiyo si tu inalinda mali zao bali pia inachochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Aidha, amesema Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kusimamia sera za fedha kwa weledi ili kudumisha utulivu wa uchumi, kuvutia uwekezaji na kuhakikisha mfumo wa kifedha unaendelea kuwa imara kwa manufaa ya wananchi wote.

Post a Comment

0 Comments

TUTUBA: BODI YA BIMA YA AMANA, NGAO YA USALAMA WA FEDHA ZA WANANCHI