UMMY: TAASISI ZIHAKIKISHE WATU WENYE ULEMAVU WANASHIRIKISHWA KIKAMILIFU


NA ASHA MWAKYONDE, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, amezitaka taasisi za umma na binafsi kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa nafasi sawa za kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa kuondoa vikwazo vinavyowazuia kupata huduma na fursa mbalimbali.

Akizungumza leo Julai 6,2026 alipotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), "Sabasaba" Ummy amesema ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu unapaswa kuanza katika utoaji wa huduma, ajira na mawasiliano yanayozingatia mahitaji yao.

Amesema ni muhimu kwa taasisi na kampuni kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na huduma ili yawe rafiki kwa watu wenye ulemavu, hatua ambayo itawawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aidha, amewataka wadau wote kuendelea kujifunza na kuongeza uelewa kuhusu haki za watu wenye ulemavu ili kuhakikisha hakuna anayebaguliwa kutokana na hali yake.

Ummy pia ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usawa na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, akisisitiza kuwa ushirikishwaji wa kila mwananchi ni msingi wa maendeleo jumuishi nchini.

Pia Naibu Waziri huyo alitembelea banda la Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania ( SHIVYAWATA) pamoja na banda la Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC),amesema ameridhishwa na kiwango cha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maonesho ya mwaka huu, akibainisha kuwa ushiriki huo umeongeza fursa za kiuchumi na kuwajengea kujiamini zaidi.

Naibu Waziri Nderiananga ameeleza kuwa Serikali imegharimia ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maonesho hayo bila wao kubeba gharama yoyote, hatua iliyowapa nafasi ya kutangaza bidhaa zao na kufanya biashara katika mazingira yenye usawa na heshima na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha ushiriki huo katika miaka ijayo ili watu wengi zaidi wenye ulemavu wanufaike na fursa hizo.

Post a Comment

0 Comments

UMMY: TAASISI ZIHAKIKISHE WATU WENYE ULEMAVU WANASHIRIKISHWA KIKAMILIFU