USHIRIKIANO BAINA YA TAASISI NI MUHIMU KWA MAENDELEO - WAZIRI OMAR


Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM 

WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uratibu na uhusiano kati ya taasisi mbalimbali za Serikali (link by coordination) ili kuboresha utekelezaji wa mipango ya maendeleo, hususan katika Mkoa wa Dodoma.

Waziri Omar ametoa kauli hiyo leo Julai 02,2026 alipotembelea banda la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu 'Sabasaba' ambapo ameeleza kuwa maendeleo ya wananchi yataimarika zaidi endapo kutakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi zinazotekeleza mipango ya maendeleo.

Amesema Chuo cha Mipango kimekuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha wataalamu wa mipango ambao wengi wao huajiriwa na kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, hatua inayosaidia kupunguza uhaba wa wataalamu wa sekta hiyo nchini.

Aidha, ametaka kufahamu kama chuo hicho kinajikita zaidi katika kupanga mipango ya watu au pia kinahusisha mipango ya miji, akisisitiza umuhimu wa kuendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo ya miji na vijiji.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti na Machapisho wa IRDP, Dk. Africanus Sarwatt, amesema chuo hicho kinatoa programu mbalimbali kuanzia ngazi ya stashahada hadi shahada ya uzamili, zikiwa zimejikita zaidi katika masuala ya maendeleo ya vijijini na mipango ya maendeleo kwa ujumla.

Amesema awali chuo kilijikita zaidi katika kupanga mipango ya watu, lakini kadri mahitaji ya maendeleo yalivyoongezeka, kimejikita pia katika mipango miji ili kukidhi changamoto za ukuaji wa miji na vijiji.

Dk. Sarwatt ameongeza kuwa chuo hicho pia kimeanzisha programu za TEHAMA ili kuchunguza namna teknolojia inavyoweza kuchangia maendeleo ya vijijini na kuboresha utoaji wa huduma za mipango.


Amesema wahadhiri wa chuo hicho huchapisha tafiti mbalimbali kupitia majarida ya kitaaluma (journal articles), pamoja na vitabu na machapisho mengine ya kisayansi, yanayolenga kuongeza uelewa kwa jamii na wataalamu.

“Tunachapisha tafiti zetu kupitia majarida ya kitaaluma na pia kupitia vitabu mbalimbali, pamoja na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii kama njia ya kuelimisha jamii na kujitangaza kitaaluma,” amesema.

Dk. Sarwatt ameeleza kuwa chuo hicho pia kinashiriki moja kwa moja kusaidia Mkoa wa Dodoma na wilaya zake katika kupanga na kuboresha mipango ya maendeleo ya maeneo ya mijini na vijijini.

Ameongeza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa chuo hicho ni kupunguza uhaba wa wataalamu wa mipango nchini, hususan katika sekta ya maendeleo ya vijijini.

Post a Comment

0 Comments

TPDC YAELEZA MAFANIKIO YA UTAFITI WA MAFUTA NA GESI SABASABA