TPDC YAELEZA MAFANIKIO YA UTAFITI WA MAFUTA NA GESI SABASABA

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),limesema linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya utafiti wa mafuta na gesi kwa kutumia fedha za ndani zinazotengwa na Serikali, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza upatikanaji wa nishati na kukuza uchumi wa Taifa.

Hayo yameelezwa leo Julai 2,2026 na Mjiolojia wa TPDC, Magambo Samweli, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba

ambapo amesema lengo la ushiriki wa shirika hilo ni kutoa elimu kuhusu majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 pamoja na miradi ya utafiti inayotekelezwa nchini.

Amesema miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea ni mradi wa utafiti wa Bonde la Eyasi-Wembere, unaohusisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida, Manyara na kuelekea Arusha.

Kwa mujibu wake, TPDC inaendelea na hatua za ukusanyaji wa taarifa za mitetemo (2D seismic survey), ili kuchunguza miamba iliyo chini ya ardhi na kubaini kama ina uwezo wa kuzalisha na kuhifadhi mafuta au gesi.

"Jiolojia ya Bonde la Eyasi-Wembere inafanana kwa kiasi kikubwa na maeneo ya Uganda ambako mafuta yaligunduliwa, hivyo tuna matumaini makubwa kwamba utafiti huu unaweza kuzaa matokeo chanya," amesema.

Amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa data ilifanyika mwaka 2022 ambapo takribani kilomita 250 za taarifa za mitetemo zilikusanywa, huku awamu ya pili ikiendelea kwa lengo la kukusanya takribani kilomita 1,100 za data kabla ya kuendelea na hatua zinazofuata za utafiti.

Aidha, amesema TPDC inajiandaa kuanza mradi mwingine wa utafiti katika kitalu cha Songosongo Mashariki, ambapo bajeti ya utekelezaji tayari imeidhinishwa na Serikali na shughuli za ukusanyaji wa data zinatarajiwa kuanza mwaka ujao.

Ameleza kuwa utafiti huo unalenga kuongeza taarifa za kijiolojia katika eneo hilo ambalo tayari linazalisha gesi asilia inayosafirishwa kupitia bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Samweli amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya shughuli za utafiti wa mafuta na gesi ili kupunguza hatari za uwekezaji na kuvutia wawekezaji kushiriki katika maendeleo ya sekta hiyo.

Ameongeza kuwa hadi sasa TPDC imefanikiwa kugundua gesi asilia pekee, huku jitihada zikiendelea za kutafuta na kugundua mafuta nchini kupitia miradi mbalimbali ya utafiti.

"Malengo yetu ni kuendelea kuongeza rasilimali za nishati kwa manufaa ya maendeleo ya uchumi wa taifa na kuhakikisha Watanzania wananufaika na sekta ya mafuta na gesi," amesema.

Post a Comment

0 Comments

MAHUNDI AWASILI SONGEA KWA KONGAMANO LA KUWAWEZESHA WANAWAKE