WAZIRI OMAR AIPONGEZA NBS KWA KUHIFADHI TAKWIMU KIDIJITALI

Na Asha Mwakyonde DAR ES SALAAM 

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imepongezwa kwa kuendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, hatua inayorahisisha upatikanaji wa takwimu rasmi za Tanzania kwa wananchi, watafiti, wawekezaji na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, baada ya kutembelea banda la NBS katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alipata fursa ya kuona maendeleo yaliyofikiwa na taasisi hiyo katika kuhifadhi na kusambaza takwimu kupitia mifumo ya kidijitali.

Waziri Omar amesema matumizi ya teknolojia yamekuwa nyenzo muhimu katika upatikanaji wa taarifa kwa wakati, hivyo juhudi za NBS za kuweka machapisho yake yote katika mfumo wa kidijitali zitachangia kuongeza upatikanaji wa takwimu sahihi na zinazotegemewa kuhusu Tanzania.

Amesema katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia, watu wengi hupata taarifa kupitia majukwaa ya mtandaoni na mifumo ya akili bandia (AI), hivyo uwepo wa takwimu rasmi za NBS kwenye mifumo hiyo utaongeza uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusu nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NBS, Spika Mstaafu Anna Makinda, amesema taasisi hiyo inaendelea na maandalizi ya sera itakayoboreshwa ili kuendana na mahitaji ya sasa katika upatikanaji na matumizi ya takwimu rasmi nchini.

Amesema sera hiyo inaandaliwa kwa ushirikiano kati ya NBS na Wizara ya Fedha kwa lengo la kuhakikisha matumizi ya takwimu yanaendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya watumiaji.

Naye Mkutubi wa NBS, Issa Magabiro, amesema taasisi hiyo inaendelea kubadilisha machapisho ya zamani kutoka nakala ngumu kwenda katika mfumo wa kidijitali.

Amesema zoezi hilo linahusisha machapisho yote ya takwimu yaliyotolewa kuanzia mwaka 1938 hadi sasa, ambapo yale yaliyokuwa tayari katika mfumo wa kielektroniki yamehifadhiwa mtandaoni, huku mengine yakiendelea kufanyiwa uchakataji wa kidijitali.

Magabiro amesema mpango huo utawezesha watafiti, wawekezaji, taasisi mbalimbali na wananchi kupata takwimu rasmi kwa urahisi zaidi, sambamba na kuimarisha uhifadhi wa kumbukumbu muhimu za takwimu za Taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Post a Comment

0 Comments

MAHUNDI AWASILI SONGEA KWA KONGAMANO LA KUWAWEZESHA WANAWAKE