Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
OFISI ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) imesema inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwa kushughulikia kwa haraka malalamiko yanayohusu kodi, hatua inayochochea ulipaji wa kodi kwa hiari na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza Julai 2, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Erastus Mtui, alisema ofisi hiyo imeshiriki maoneshoni humo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake, kupokea malalamiko ya kikodi na kuwasaidia walipakodi kupata ufumbuzi wa changamoto wanazokutana nazo.
Alisema tangu kuanza rasmi shughuli zake takribani miaka miwili na nusu iliyopita, ofisi hiyo imekuwa kiungo muhimu kati ya walipakodi na mamlaka za kodi kwa kuhakikisha changamoto zinazowasilishwa zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Mtui alisema lengo la kuanzishwa kwa ofisi hiyo ni kuhakikisha mfanyabiashara au mwekezaji anayekutana na changamoto za kikodi anapata mahali salama pa kuwasilisha malalamiko yake ili yashughulikiwe kwa haki na kwa wakati.
"Kodi ni msingi wa maendeleo ya nchi. Tunawahimiza walipakodi kutekeleza wajibu wao kwa hiari, nasi tupo kuhakikisha changamoto zinazoweza kuwazuia kufanya hivyo zinapatiwa suluhisho," alisema.
Alibainisha kuwa ofisi hiyo ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuwa mazingira bora ya biashara na uwekezaji yanasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi unaolengwa kufikia asilimia 10, na hatimaye kujenga uchumi wa dola trilioni moja.
Aidha, alisema wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa kufika katika ofisi za taasisi hiyo, kupiga simu za bure, kutumia mfumo wa mtandao au programu ya Suluhu ya Kodi App kwa watumiaji wa simu janja.
Aliongeza kuwa maandalizi ya mfumo wa USSD yamekamilika na utazinduliwa ili kuwawezesha pia wananchi wanaotumia simu zisizo janja kuwasilisha malalamiko yao kwa urahisi zaidi.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, Mtui alisema katika kipindi cha miaka miwili na nusu, ofisi hiyo imepokea na kushughulikia jumla ya malalamiko 593, huku malalamiko 340 yakipokelewa na kushughulikiwa katika mwaka uliopita pekee.
Aliwataka wananchi kutembelea banda la Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na kufahamu njia mbalimbali za kuwasilisha malalamiko ya kikodi.

0 Comments