Na Asha Mwakyonde DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ametembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amejionea huduma zinazotolewa na taasisi hiyo pamoja na mchango wake katika kulinda amana za wateja na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha nchini.
Balozi Omar ametembelea banda hilo leo Julai 02,2026 katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), 'Sabasaba' alipokelewa na viongozi na watumishi wa DIB waliompa maelezo kuhusu majukumu ya bodi hiyo, huduma inazotoa na jitihada zinazofanywa kuelimisha umma kuhusu Mfumo wa Bima ya Amana.
Katika maelezo hayo, Waziri amepata fursa ya kufahamu namna DIB inavyolinda amana za wateja wa benki na taasisi za fedha, pamoja na nafasi yake katika kuimarisha utulivu na uaminifu wa sekta ya fedha nchini.
Akizungumza katika maonesho hayo, Ofisa Mwandamizi wa DIB, Joyce Shala, amesema Bodi hiyo imeongezewa jukumu la kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza wakati wa utatuzi wa migogoro au changamoto katika uendeshaji wa taasisi za fedha.
Shala amesema DIB pia imepiga hatua katika kulipa fidia kwa wateja wa iliyokuwa Benki ya FBME, ambapo hadi sasa imefanikiwa kuwalipa asilimia 85 ya wateja wanaostahili.
Amefafanua kuwa malipo hayo yalifanyika kwa awamu mbalimbali, zikiwemo asilimia 35 katika awamu ya kwanza, asilimia 28 katika awamu ya pili na asilimia 22 katika awamu ya tatu, na kufikisha jumla ya asilimia 85.


0 Comments