Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili–Mloganzila imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa na ubobezi kwa kutoa huduma ya kupunguza uzito kwa njia ya puto (Intragastric Balloon), ambapo watu zaidi ya 186 wamenufaika na huduma hiyo tangu ilipoanza kutolewa hospitalini hapo Novemba 2022.
Akizungumzia huduma hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji Eric Muhumba amesema huduma hiyo imekuwa suluhisho salama na yenye matokeo chanya kwa watu wenye changamoto ya uzito uliopitiliza.
Kwa mujibu wa Dkt. Muhumba Muhimbili–Mloganzila imeendelea kuboresha huduma hiyo kwa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na kuwahusisha wataalamu wa lishe na mazoezi ya mwili ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma jumuishi zinazowawezesha kufikia na kuwa na uzito unaofaa kwa afya bora.
Aidha, amesema huduma hiyo imevutia watu kutoka ndani na nje ya Tanzania kutokana na ubora wake ambapo hadi sasa hospitali imeshatoa huduma hiyo kwa wagonjwa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Malawi.
Ameongeza kuwa hospitali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha huduma mpya za kupunguza uzito kwa kutumia sindano na vidonge.
Mbali na huduma ya kupunguza uzito kwa njia ya puto, Dkt. Muhumba amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kibingwa na ubobezi katika upasuaji, zikiwemo upasuaji wa matundu madogo, upasuaji wa saratani za koo, saratani za kongosho pamoja na upasuaji rekebishi.


0 Comments