VETA TANGA YAWAJENGEA VIJANA UJUZI WA KUJIAJIRI

Na Asha Mwakyonde, RUKWA 

MAFUNZO ya ufundi stadi yanaendelea kuwa fursa muhimu kwa vijana kujikwamua kiuchumi kupitia kujiajiri, huku wahitimu wakihitaji pia mitaji na vifaa ili kutumia ujuzi walioupata kuanzisha biashara zao.

Akizungumza leo Oktoba 12,2026 katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika mkoani Rukwa, yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”Mhitimu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Tanga, Ernest Igobeko, amesema mafunzo ya useremala aliyopata chuoni hapo yamemwezesha kufanya kazi mbalimbali na kujipatia kipato, ingawa bado hajafanikiwa kuwa na karakana yake binafsi.

Igobeko amesema tangu alipohitimu amekuwa akitengeneza bidhaa mbalimbali za mbao, zikiwemo viti, meza, makabati na vitanda, lakini kwa sasa anafanya kazi chini ya mtu mwingine kutokana na kutokuwa na mtaji wa kuanzisha karakana yake.

Amebainisha kuwa ujuzi alioupata umemsaidia kupiga hatua katika maisha na kupunguza utegemezi, huku akieleza kuwa kupata mtaji kutamwezesha kufungua karakana yake na kupanua shughuli zake za kiuchumi.

“Ninaomba wadau mbalimbali wanisaidie ili niweze kufungua karakana yangu. VETA imenipatia ujuzi unaoweza kunisaidia kujitegemea, hivyo nikifanikiwa kupata eneo na vifaa vya kufanyia kazi, nitaweza kupanua shughuli zangu,” amesema Igobeko.

Akizungumzia mafunzo ya useremala yanayotolewa chuoni hapo,ameeleza kuwa wanafunzi hujifunza mbinu mbalimbali za kutengeneza samani, kuunganisha mbao na kutumia vifaa vya kazi kwa usahihi ili kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Amesema mafunzo hayo yanahusisha pia utambuzi wa aina mbalimbali za mbao na sifa zake, jambo linalowasaidia wanafunzi kuchagua malighafi inayofaa kulingana na bidhaa wanayotaka kutengeneza.

"wanafunzi hufundishwa mbinu za kukereza mbao, kutengeneza miguu ya meza na viti pamoja na kufanya mapambo yanayoongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa," amesema.

Amesema kuwa ujuzi huo ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazohitajika majumbani, maofisini na katika maeneo mengine, huku ukiwawezesha kutumia maarifa yao kuanzisha shughuli za kujipatia kipato.

Ameongeza kuwa katika mafunzo hayo, wanafunzi pia hujifunza namna ya kutumia malighafi kwa ufanisi ili kupunguza upotevu na kuongeza thamani ya mbao zinazotumika katika utengenezaji wa samani.

Amebainisha kuwa VETA Mkoa wa Tanga inaunga mkono juhudi za kuwawezesha watu wenye mahitaji maalumu kupata mafunzo ya ufundi stadi, ikiwemo kutoa fursa za mafunzo kwa utaratibu unaolenga kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu hiyo.

Igobeko amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa watu wenye mahitaji maalumu wanapata nafasi ya kujifunza ujuzi unaoweza kuwasaidia kujiajiri, kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kujitegemea kiuchumi.

Aidha, ameeleza kuwa mafunzo ya ufundi stadi yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa baadhi ya vifaa vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi pale vinapoweza kutengenezwa ndani ya nchi kwa kutumia ujuzi na teknolojia inayopatikana.

Kwa upande wa utunzaji wa mazingira, amesema matumizi bora ya mbao na mabaki yake katika utengenezaji wa samani yanaweza kupunguza upotevu wa malighafi na kuongeza thamani ya rasilimali zinazotumika katika shughuli za uzalishaji.

Aidha amefafanua kuwa VETA Mkoa wa Tanga inatoa fursa kwa wananchi, wakiwemo vijana na watu wenye mahitaji maalumu, kujitokeza kupata mafunzo ya ufundi stadi yatakayowawezesha kutumia ujuzi wao katika kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii.

Ushuhuda wa Igobeko unaonesha kuwa pamoja na mafunzo na ujuzi unaopatikana chuoni, upatikanaji wa mtaji na vifaa vya kazi ni miongoni mwa mahitaji yanayoweza kuwasaidia wahitimu kuanzisha biashara zao na kupanua fursa za ajira.

Post a Comment

0 Comments

PPRA YANG'ARA KILELE MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026