Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KASI ya mabadiliko ya teknolojia na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii limeibua umuhimu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuimarisha mifumo ya usimamizi wa uchaguzi ili kuhakikisha maendeleo ya kidijitali yanakuwa chachu ya demokrasia badala ya kuwa chanzo cha migawanyiko na upotoshaji wa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka tume za uchaguzi za nchi wanachama wa SADC kutumia ipasavyo teknolojia, mitandao ya kijamii na akili unde (AI) katika kuboresha usimamizi wa uchaguzi na kuimarisha demokrasia katika ukanda huo.
Amesema teknolojia za kisasa zina nafasi kubwa katika kuboresha mawasiliano, kutoa elimu kwa wapiga kura na kusambaza taarifa zinazohusu michakato ya uchaguzi kwa wakati, lakini ni muhimu kuweka mikakati ya kukabiliana na matumizi yake yasiyo sahihi, hususan usambazaji wa taarifa potofu.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 28 wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa SADC (ECF-SADC), uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency – The Kilimanjaro.
Amesema taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kwa kasi wakati wa uchaguzi zinaweza kusababisha migawanyiko katika jamii, kuathiri taswira ya taasisi za uchaguzi na kupunguza imani ya wananchi katika michakato ya kidemokrasia.
“Kwa kuwa uchaguzi ni zoezi lenye hamasa kubwa kwa jamii, taarifa zisizo sahihi zinaposambazwa kwa kasi zinaweza kuwa na athari hasi na hata kusababisha migawanyiko katika jamii, kuathiri taswira ya taasisi za uchaguzi na kupunguza imani ya wananchi katika michakato ya kidemokrasia,” amesema.
Kuhusu matumizi ya akili unde, Waziri Mkuu amezitaka tume hizo kuendelea kujenga uwezo wa kutumia teknolojia hiyo ambayo inaendelea kukua na kubadilika kwa kasi, ili ziweze kukabiliana na changamoto zake na kutumia fursa zinazotokana na maendeleo yake.
Amesisitiza kuwa usimamizi imara wa uchaguzi ni msingi muhimu wa kukuza demokrasia na ustawi wa jamii, hivyo nchi za SADC zinapaswa kuendelea kuimarisha mifumo ya uchaguzi inayozingatia sheria, kanuni na misingi ya kidemokrasia.
Mkutano huo wa siku tatu unajadili usimamizi wa uchaguzi katika zama za mitandao ya kijamii na namna ya kuimarisha wajibu wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi katika ukanda huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amesema ushiriki wa Tanzania katika ECF-SADC tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998 umeiwezesha nchi kupata fursa za kujifunza na kubadilishana uzoefu na tume nyingine za uchaguzi.
Amesema ushirikiano huo umekuwa na mchango katika kuimarisha mifumo ya uchaguzi na kujenga uwezo wa taasisi zinazohusika na usimamizi wa uchaguzi.
Naye Rais wa Jukwaa la ECF-SADC, Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva, amesema jukwaa hilo lina jukumu la kuimarisha uhuru, kutopendelea upande wowote na kukuza weledi wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi katika nchi wanachama.
Ameongeza kuwa jukwaa hilo pia linatoa fursa ya kujifunza mbinu mpya za usimamizi wa uchaguzi na kujenga mahusiano ya kikazi baina ya taasisi hizo hata katika vipindi ambavyo nchi husika hazifanyi uchaguzi.
Mkutano huo umewakutanisha wenyeviti, makamishna, wakurugenzi na watendaji wa tume za uchaguzi kutoka nchi wanachama wa SADC kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa uchaguzi, changamoto za teknolojia na nafasi ya mitandao ya kijamii katika michakato ya kidemokrasia.






0 Comments