Na Asha Mwakyonde,Dodoma
KUNA msemo usemayo hujafa hujaumbika, msemo huu unadhihirika kwa Habiba Athumani (48),mkazi wa Maili Mbili Wilaya ya Dodoma, jijini hapa ambaye alianza kuumwa mwaka 2010 na kusababisha kushindwa kufanya shughuli zake za kumuingizia kipato.
Habiba ni mama wa watoto wa nne wanaomtegemea ambapo pamoja na kuugua mume wake alimtelekeza na familia hiyo lakini pia anategemewa na familia yake akiwamo mama yake mzazi ambaye anamuuguza.
Viongozi na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Dodoma (DWJ),walimtembelea Habiba ili kujua changamoto zinazomkabili, ambapo ameanza na historia ya kuugua kwake amesema alikuwa amekaa nyumbani akahisi miguu inakosa mawasiliano.
Lengo la DWJ ni kuisaidia jamii hasa kuhakikisha wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo wanarudi na kuendelea na masomo yao.
Akizungumza na DWJ Habiba ameeleza kuwa baada ya dakika kama kumi mikono nayo ilianza kukosa mawasiliano ndipo mikono yake ikaanza kujikunja na kukakamaa na kujikunjia kifuani.
"Sina uwezo wa kunyoosha mikono wala kufanya chochote nilikaa pale nyumbani, kuamka asubuhi miguu nayo ikaishiwa nguvu nikawa siwezi kutembea.
Kutokana na hali hiyo Habiba ameeleza kuwa alikuwa ni mtu wa kupelekwa chooni ,kurudi ndani na kuhudumiwa kila kitu huku akisema hana msaada wa aina yoyote hivyo amewaomba watanzania kumsaidia kwa kuwa anateseka.
Habiba ameongeza kuwa mkono wake kulia umepooza lakini pamoja na kupooza anaenda kufanya vibarua vya kufua nguo za watu ili aweze kuihudumia familia yake ikiwa ni pamoja na mtoto wake wa kiume anaesoma katika Chuo Cha Nyuki mkoani Taboara.
Amesema kuwa amekaa kitandani kwa muda wa miaka sita bila ya kutembea baada ya kupooza mwili na kwamba ilipofika mwaka 2017 aliweza kutembea tena kutokana na matibabu aliyoyapata hospitali katika Hosptali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Habiba akizungumzia Maisha aliyokuwa anaishi jijini Dar es salaam wakati akiendelea kuhudumia Muhimbili amesema kuwa alifikia kwa wasamaria wema lakini baadae baba wa watoto wake limpangia chumba ambapo alikaa na mtoto wake huku akifanya biashara ya kupika vitumbua .
"Sikuwa na msaada wowote, baba wa watoto wangu alinipangia tu chumba basi nikaanza kupika ili niweze kupata hela ya kula na nauli ya kwenda hospialini Muhimbili," amesema.
Mama yake Habiba
Habiba amefafanua kuwa mkono wake wake wa kulia ni changamoto inayompa wakati mgumu kufanya kazi kwa ufanisi ili kuhudumia familia yake.
"Pamoja na kuihudumia familia yangu mimi mwenyewe ni mgonjwa mama yangu mzazi huyu hapa, mwaka 2020 alianguka akavunjika mguu. Tukamuuguza akapata nafuu baada ya mama kupata nafuu, mwanangu wa chuo naye akaanza kuumwa kumbe alikuwa na uvimbe tumboni," amesema Habiba.
Habiba akiongea kwa masikitiko na huzuni amesema hakuwa na uwezo wa fedha hali iliyomsababisha kuomba msaada huku na kule ili mwanaye aweze kufanyiwa upasuaji na baadae hospitali walikubali kumfanyia upasuaji.
Akizungumza huku analia, Habiba ameeleza kuwa baadae mama yake alianguka kwa mara ya pili na kuvunjika mguu ule ule wa mwanzo.
AFYA YA WATOTO WAKE
Mbali na hilo,Habiba amezungumzia afya ya watoto wake nakusema kuwa
wanakabiliwa na changamoto ya hali za kiafya ambapo mtoto wake wa kwanza aliyekuwa anamtegemea anasumbuliwa na uvimbe kwenye koo huku mwingine akisumbuliwa na matatizo ya akili.
’’Ninavyoongea hivi sasa baba yangu yupo nyumbani anaumwa sana nashindwa hata kuhadithia, ana watoto wa kiume lakini hawamjali kwa lolote ,anaweza akajisaidia akakaa na haja kubwa na ndogo siku mbili ndani. Sina msaada wa aina yoyote ,mimi ndo kama mnavyoniona, mtoto wa shule anasoma kwa shida chuoni kula kwake ni shida," amesema.
Ameongeza kuwa ada ya mtoto wake anaipata kwa kukopa hela kwa watu wanaomuamini kwa kipindi cha miaka mitatu sasa na kwamba hajui atazirejeshaje kutokana na hali halisi ya maisha yake ilivyo.
Habiba amesema kuwa tangu aanze kuugua amekuwa ni mtu wa kufukuzwa kila anapoishi kwa kushindwa kulipa madeni ya watu sambamba na kodi ya nyumba (analia), na kwamba kuna muda anatamani kufa ili kuepukana na kadhia hizo.
"Madeni yamenijaa nina daiwa Pamoja na hali yangu ya mkono wangu kuwa na changamoto lakini ninafua mashuka ya watu na mkono wangu mmoja ili nipate pesa ya kuhudumia familia yangu," ameeleza.
Amesema kuwa anafua nguo za watu ili kujipatia riziki lakini mkono huo muda mwingine unakosa nguvu na kwamba akiendelea akifua nguo nyingi kidole kinaniuma kwa sababu hapo kwenye mkono wake wa kulia kidole cha ndani kucha yake huwa inatoka.
Kwa mujibu wa Habiba "Nikishika maji hii kucha huwa inaoza inatoka na inaota nyingine nikishika maji inaoza yaani ndo maisha yangu yote.Matumaini yangu makubwa hivi sasa ni kwa watanzania kunisaidia ili niondokane na changamoto hizi zinazo nikabili," amesema.
AOMBA MSAADA KWA WATANZANIA
Kwa atakaye guswa kumsaidia Habiba anaweza kumpata kupitia 0763987358 Namba yake ya simu ya mkononi.
Anawaomba Watanzania kumsaidia ili alipe madeni ya watu, kupata sehemu ya kukaa, kujengewa chumba kimoja kwa kuwa anakiwanja Pamoja na kupata biashara ambayo inamuepusha kuwa omba omba kwa jamii iliyomzunguka.
0 Comments