Na Asha Mwakyonde,Dodoma
KAIMU Meneja Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Nchini kutoka Wizara ya Afya, Dk.Peter Neema amesema kuwa maendeleo ya utoaji wa huduma ya Kifua Kikuu na Ukoma yafikia asilimia 32 kati ya malengo ya asilimia 50 ya mpango huo ifikiapo mwaka 2025 ambapo umeonekana kufanya vizuri kwenye eneo la uibuaji wa wagonjwa, maambukizi wapya.
Akizungumza jijini Dodoma Feburuari 10,2023, wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya zoezi la tathimini, mpango mkakati wa sita wa Kifua Kikuu na ukoma nchini Dk. Neema amesema mpango huo umeweza kufikia asilimia 32 katika kupunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo asilimia 55 kati ya lengo la asilimia 75.
Dk. Neema akizungumzia changamoto katika uibuaji ambapo hadi sasa wameweza kuibua asilimia 65 kati ya ile ambayo wanatakiwa kuibua na kwamba wana kazi ya kukamilisha asilimia 35 iliyobaki.
Meneja huyo amefafanua kuwa zoezi hilo lilianza kufanyika yangu Januari 30 hadi Februari 10 na kwamba tathimini hiyo ilianza kwa vitendo kukusanya takwimu na kuangalia maendeleo ya utoaji Huduma za kifua Kikuu na ukoma ikiwa ni pamoja na kuandika ripoti ambapo wamekamilisha Februari 9, mwaka huu.
Ameongeza kuwa wamekuwa na changamoto ya wangonjwa ambao wanaibuliwa wamekuwa wakiwaibua kwa kutumia dalili huku akissema bado wanakazi ya kufanya ili kuweza kuwafikia wagonjwa wengi kwa kutumia vipimo vya kimaabara.
"Mpango unafanya mkakati wa kuongeza mashine za kupima vinasaba vya kupima Kifua kikuu tuweze kufikia lengo la uibuaji angalau asilimia 90 na kwa sasa tupo asilimia 65,pia tuna mkakati wa kuongeza vituo vya kimaabara na kushirikiana na jamii kwa kutoa elimu ya njia bora ya ukusanyaji makoozi pamoja na njia mbadala za uibuaji," amesema.
Dk. Neema ameeleza kuwa kwa sasa wanatarajia kufanyia maboresho mpango mkakati wao wa sita ili kuchukua maoni yaliyotolewa katika ripoti hiyo kwa lengo la kufikia malengo yao itakapofika mwisho wa utekelezaji wao mwaka 2025.
Amesema kuwa tathimini hiyo imefanywa kwa jicho la pili (External Reviews), ambapo wametoka nje ya nchi na baadhi yao ni kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID),na Stop Tv PartnerShip na kwamba kutoka nje nchi walikuwa 18, timu ya wataalam wa ndani,wadau wa nao wameshiriki pamoja na taasisi za Serikali ili kuweza kutathimini mpango huo.
Naye Msimamizi Mkuu wa Huduma za Uhakiki,Tathimini na Kifua Kikuu kutoka Shirika lisilo la kiserikali (SHDEPHA+) lililopo wilayani kahama Mkoa wa Shinyanga, Rabia Khaji amesema kuwa Mkoa huo upo hatarini watu wake kupata Kifua Kikuu kutokana na kuzungukwa na migodi na wengi kufanya Shughuli zao katika migodi hiyo.
"Tunahitaji huduma hizi ili ziweze kuwafikia makundi ya watu hawa ambao wanajishughulisha na kazi za uchimbaji madini, kwa Kahama madini ni sehemu inayochangia ukuaji wa uchumi," amesema.
Ameongeza kuwa ili kuwafikia watu hao wanawatumia wahudumu ngazi ya jamii ambao wanatoka katika kundi la wachimbaji na wamesaidia kwenda kutoa elimu ya Kifua Kikuu na kufanya uchunguzi wa awali na kuweza kubaini dalili ambazo zinawasumbua kama kukohoa, kupata jasho wakati wa usiku, kukohoa, kuchemka na kupungua uzito.
Ameeleza kuwa baada ya kuwabaini wenye dalili za awali wanapa Rufaa kwenda kufanyiwa uchunguzi zaidi na wanaopatikana wanapatiwa matibabu.
Amefafanua kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa kwa kuleta digital mobile van Kliniki ambapo imekuwa ni chagizo kubwa ambayo imeweza kuwafikia wachimbaji wengi na kutoa huduma za upimaji wa Ukimwi panapokuwa na huduma hizo za upimaji huo wa Kifua Kikuu zinapofanyika.
0 Comments