Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro amesema kuwa Mpango wa Uwekezaji Mahiri (SWICA),unalenga kuongeza mapato kwa kuwa dhana yake ni kuvutia uwekezaji mkubwa wa miaka 30.
Pia amesema serikali inatarajia kukusanya wastani wa Dola za kimarekani 9,485,000 sawa na bilioni 22.1, kwa mwaka na kwamba mapato hayo ni mara 13 ya wastani wa mapato yaliyokuwa yanapatikana kwa mwaka katika uwekezaji wa uwindaji wa kitalii katika vitalu.
Dk.Ndumbaro aliyasema hayo juzi jijini Dodoma katika hafla ya kutunuku vyeti vya uwekezaji mahiri wa mpango wa SWICA kwa kampuni nne zilizofanya vizuri kwenye shughuli za Uutalii alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA),imefanya ubunifu mkubwa na wa kuigwa na Taasisi zilipo chini ya wizara hiyo.
Alisema kuwa uwekezaji huo unalenga zaidi watu mashuhuri kutoka maeneo mbalimbali Duniani na unato fursa ya kuchanganya shughuli za kitalii katika kitalu kimoja.
Waziri hiyo alizitaja kampuni hizo zilizotunukiwa vyeti kuwa ni Grumet Reserves Ltd, Mkwawa Hunting Safaris Ltd, Mwiba Holdings Ltd na Greet Mile Safari Campany Ltd.
" Tumekutana siku ya leo katika tukio la kihistoria la kutunuku vyeti vya uwekezaji waliokidhi vigezo vya uwekezaji katika maeneo ya uwekezaji mahiri kwa shughuli za utali," aliongeza.
Niungane na wazungumzaji waliotangulia kuipongeza TAWA kwa hatua hii iliyofikia na kuhamasisha wawekezaji mahiri kuwekez katika maeneo uwekezaji mahiri," alisema Dk. Ndumbaro.
Aliongeza kuwa mpango huo wa SWICA unakwenda sambamba na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapindizi (CCM), na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano ambao unaelekeza kuongeza watalii kutoka 1,527,230 hadi 5,000,000 na mapato kutoka Dola za kimarekani bilioni 2.6 hadi kufikia Dola bilioni 6 ambayo pia inaelekeza kujenga mazingira wezeshi kuvutia ya uwekezaji.
Awali Mwenyekiti wa bodi ya TAWA Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko alisema Matarajio yao ni ukusanyaji wa zaidi ya Tsh.Bilioni 23 kwa mwaka kutokana na uwekezaji wa kampuni hizo 4 kwenye nyanja ya uwindaji na utalii.
Aliongeza kuwa Bodi hiyo itaendelea kusimamia vyema katika kuhakikisha mapato yatokanayo na wanyamapori yanawanufaisha watanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kutunukiwa vyeti hivyo mwakilishi kampuni ya Green Mile Safari Ltd, Selem Baileith alisema atajitahidi katika kuimarisha uwindaji na uhifadhi wa wanyamapori.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mwiba Holdings Ltd Abdulkadir Mohamed alisema wazawa wanaweza katika masuala mazima ya uwekezaji wa uwindaji na uhifadhi wa wanyamapori katika sekta ya utalii.
0 Comments