Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), (Kushoto),akisaini mkataba wa makubaliano na moja ya kampuni yenye miradi ya kimkakati na mahiri ya Taifa Ges (Kulia),Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo,Hamisi Ramadhani akitia saini ya makubaliano ya utekelezaji wa mradi unaotekelezwa nchi nzima.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC),leo kimesaini makubaliano ya uwekezaji wa miradi sita ya kimkakati na mahiri ambayo itasaidia kuliingizia Taifa fedha za kigeni pamoja na Kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania.
Akizungumza jijini hapa leo Machi 25, 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dk. Maduhu Kazi, amesema miradi hiyo sita ya kimkakati na mahiri iliyochakatwa na kupitishwa na kamati ya Taifa ya uwekezaji (NISC), baada ya kujiridhisha na kukidhi vigezo vilivyoainishwa na kamati hiyo.
Amesema miradi hiyo sita ya kimkakati na mahiri ambayo ni muhimu kwa nchi inategemewa baada ya utekelezaji itakuwa na manufaa kwa nchi.
Dk. Kazi amefafanua kuwa mradi wa kwanza ni wa Itracom unaotekelezwa mkoani hapa ambao ni wa kiwanda cha uzalishaji wa mbolea na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 180 na kuleta ajira zipatazo 4,500 za moja kwa moja na kwamba 6,000 sio za moja kwa moja.
"Mradi huu utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani kaki sita za mbolea kwa mwaka," amesema mkurugenzi huyo.
Ameongeza kuwa mradi Bagamoyo Sugar unaotekelezwa mkoani Pwani ni wa kilimo cha miwa na kuwanda kwa ajiki ya uzalishaji wa sukari na kwamba utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 193.75 na kuleta ajira zipatazo 1,500 za moja kwa moja huku sio za moja kwa zikiwa 10,000.
"Kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari hivyo kitapunguza mahitaji ya uagizwaji wa sukari kutoka nje. Na mradi wa Taifa Gesi unaotekelezwa nchi nzima utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 62, na kuleta ajira 60 za moja kwa moja," amesema Dk.Kazi.
Amebainisha kuwa mradi wa nne ni wa Kagera Sugar unaotekelezwa mkoani Kagera pia ni wa kilimo cha miwa na kiwanda cha Sukari na kwamba utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 410 na kutengeneza ajira 10,000 na siziso za moja kwa moja 50,000.
Pia Mkurugenzi huyo amesema mradi wa tano nao ni wa miwa ambao unatekelezwa na Mtibwa Sugar mkoani Morogoro na ni wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 150.
" Kutakuwa na uwekezaji wa dola milioni 305 na kuleta ajira zipatazo 12,500. Na mradi wa sita ni wa Knauf unaotekelezwa mkoani Pwani ambao wawekezaji wake ni kutoka Ujerumani na kwamba utakuwa unazalisha Gypsum Board na gypsum powder na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 105," amesema.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa mradi huo utaleta ajira 150 za moja kwa moja na 500 ambazo si za moja kwa moja na kwamba kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba milioni 4 kwa mwaka.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa uwekezaji, viwanda na Biashara Exaud Kigahe amewataka watendaji wa TIC kuondoa ukiritimba unaofanywa kwa wawekezaji kwa kuwaondolea usumbufu wa ufuatiliaji vibali vya kuwekeza nchini.
Kigahe amesema Serikali imepanga kuwatafuta wawekezaji popote walipo kwa ajili ya kujua changamoto wanazokutana nazo kwenye sekta ya uwekezaji.
“Lazima tuboreshe huduma zetu na ndilo tatizo ambalo tupo nalo kwa muda mrefu, tunasema kilasiku Tanzania ni nchi tajiri lakini ni kwa rasilimali asilia hivyo kupitia utajiri huu lazima tuongeze thamani na kuzalisha bidhaa kupitia rasilimali hizo tulizonazo”alisema Kigahe
0 Comments