Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Mawasiliano, Teknolojia ya Habari Dk. Jimy Yonazi akizungumza na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi jijini hapa.
Katibu wa Baraza la wafanyakazi tawi la Habari na Mawasiliano TUGHE, Laurencia Masigo akizungumza wakati kikao cha baraza la wafanyakazi.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
SERIKALI kupitia wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetaja miradi miwili mikubwa inayofanywa na wizara hiyo kuwa ni kujenga mkongo wa Taifa pamoja na kujenga mfumo wa Anwani za makazi.
Hayo yamesemwa leo Machi 25 2022 jijini hapa na waziri wa Habari, Mawasiliano Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi kilicholenga kujadili mwenendo wa utekekezaji wa bajeti ya wizara kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 na Mpango wa bajeti ya wizara wa Mwaka wa fedha 2022/ 2023 na zoezi linaloendelea la Mfumo wa Anwani za makazi.
Waziri Nnauye amesema Miradi hiyo ni muhimu kuwepo na bila miradi ya Mkongo na mfumo wa Anwani za makazi sekta zingine zitashindwa kufanya kazi ipasavyo.
Amesema kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan wizara hiyo mpya ambayo ina muda mfupi mafanikio yake ni makubwa kutokana na miradi inayotekelezwa na kusimamiwa na wafanyakazi wa wizara ya habari.
Waziri huyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Ilani ya chama cha mapinduzi (CCM),walitakiwa kujenga Mfumo wa anwani za makazi kwa muda wa miaka 5 lakini imekuwa tofauti na kwamba sasa wanajenga Mfumo kwa muda wa miezi 5.
Amefafanua kuwa jambo hilo litawezekana Kama watakuwa wamoja kwani wamefika mahali pazuri ambapo tathimini inaonyesha wamefikia asilimia 30 hadi 40 na kwamba Mei 22, mwaka huu watakabidhi miradi hiyo.
"Tunapokuwa tunakabidhi Mfumo huu lazima tutambue mchango wa kila mmoja uonekane katika kuhakikisha Mfumo huu unafanikiwa kwani jambo hilo sio dogo litabaki kwenye historia ya Vizazi ,"amesema Nnauye
Akizungumzia kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia amesema wameweza kuanzishwa Mradi Mkubwa wa Tanzania ya kidigitali na wafanyakazi waote waliopewa dhamana watahakikisha Tanzania ya kidigitali inawezekana.
Aidha waziri Nnauye ametoa wito kwa Menejimenti kuhakikisha Wizara inakuwa na mazingira mazuri ya utendaji kazi pamoja na mafanikio hayo ataendelea kupigania mazingira mazuri ya wafanyakazi pamoja mahusiano mazuri kazini.
"Nitahakikisha utendaji kazi baina wafanyakazi wanapata Haki na stahili zenu zinatolewa kwa wakati. Nawataka watumishi wa wizara hii kuhakikisha wanatenda haki bila kujali Mkubwa au mdogo," ameeleza.
Nnauye amesema, kwa kuzingatia uhusiano baina ya haki na Wajibu katika kutekeleza majukumu waliojipangia ni wajibu kufahamu na kusimamia kwa ufanisi utekekezaji wa sera Mpango mkakati sheria Kanuni na miongozo, taratibu mbalimbali ikiwamo stahili za wafanyakazi pamoja na Utawala bora.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Jim Yonazi amesema kikao hicho ni kikao Cha Siku mbili na watapitia mwenendo wa bajeti ya Mwaka wa fedha 2021/2022 na pia Mwaka wa fedha 2022/23.
Pia amesema katika kikao hicho watajadiliana suala la anuani za makazi kwani suala hilo ni jukumu kubwa kwa kuhakikisha wanafanya jambo hilo kikamilifu.
Kwa Upande wake Katibu wa Baraza la wafanyakazi tawi la Habari na Mawasiliano TUGHE Laurencia Masigo, amesema Tughe hawana malalamiko Wala hoja iliyowasilishwa hiyo ni ishala nzuri inayoonyesha utulivu na amani utawala,nakuomba wafanyakazi wote wa wizara kushirikiana Ili kuleta tija kazini.
0 Comments