UDOM YAZINDUA PROGRAMU MAALUM YA USALAMA MTANDAONI


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

IMEELEZWA kuwa bara zima la Afrika wataalamu wa masuala ya usalama mtandaoni ni elfu Saba pekee huku uhitaji ukiwa ni zaidi ya wataalam milioni Nne, ambapo kutokana na upungufu huo Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wanapambana ili kuihakikishia nchi usalama mtandaoni.

Akizungumza na wanahabari Juni 4,2025 Jijini Dodoma mara baada ya kuzindua Programu Maalumu ya Usalama Mtandaoni, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka amesema watakao soma programu hiyo uwezekano wa kupata ajir nje ya mipaka ya nchi ni mkubwa.

“Na hili pia ni lengo la kitaifa kwamba vijana na wataalam kutoka hapa kwetu kushiriki katika fursa za kazi duniani kote, nadhani kwa kuanza hii programu tutafungua mlango mkubwa kwa vijana wetu anaosoma UDOM na wale wengine watakao jiunga kupata cheti ambacho kitawatambulisha kimataifa kwamba wao ni wataalamu wa masuala ya mtandao,”amesema.

Aidha, amesema fursa hiyo imetokana na Mazungumzo Kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa nchini Marekani pamoja na mojawapo wa viongozi wa Shirika hilo ambaye alimdokeza nia ya kuendelea kujenga uwezo wa nchi za Afrika katika Masuala ya Usalama Mtandaoni ambapo Rais alipendekeza kuanza na chuo hicho.


“Sisi kama chuo tunashukuru kwamba Rais wetu aliona kwamba tunaweza kuwa chuo cha kuanzia lakini lengo ni kuhakikisha kwamba watanzania wengi watashiriki ili hata badae hawa wafadhili wanaotufadhili wasipokuwepo tuweze kuendeleza wenyewe,”ameongeza.

Kwa upande wake Mratibu Mkuu wa Mradi huo Bw. Edward Sunberg, amesema hyo ni programu yao ya kwanza kuanzisha Barani Afrika na kwamba lengo ni kuona wanafunzi wengi wananufaika na mpango huo ili kukidhi vigezo vya kiushindani vya kidunia katika masuala yanayohusu usalama wa mitandao.

“Tulifanya utafiti tukagundua kuwa, ili Afrika iendelee kukua na kuwa yenye mafanikio, inahitaji sana Ulinzi na Usalama wa kimtandao. Kwa hiyo kuanzisha programu kutasaidia kuongeza wataalamu wa usalama na ulinzi wa kimtandao na kuwa msaada kwa taaluma hiyo, kwa Taifa na Afrika Kwa ujumla,”amesema.

Programu hiyo imezinduliwa kwa kuanza na awamu ya kwanza ya mafunzo yenye wanafunzi 80 wa mwaka wa Pili hadi wa Nne wanaosoma masomo ya TEHAMA, ambapo watasoma kwa mwaka mmoja na baadae wakifuzu mitihani watapata vyeti vinavyotambulika kimataifa na kusaidiwa kupata ajira.

Chuo Kikuu cha Dodoma kwa Kushirikiana na Shirika Lisilo la Kiserikali la Kimarekani Africa Program for Cyber Technology ( iACT) wamezindua mpango huo huku lengo likiwa ni kuwaongezea uwezo watalaamu wa Usalama wa Mitandao na Kuweza kutambulika Kimataifa.


Post a Comment

0 Comments

UDOSO SCHOLARSHIP FUND YAZINDULIWA