Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Athman Masasi akifafanua jambo katika kikao cha Baraza la madiwani cha kuwasilisha shughuli za utekelezaji wa maendeleo kipindi cha robo tatu ya mwaka 2021/2022.
Mwenyekiti wa kikao cha Baraza la madiwani Donald Mejiti wakati akielezea jambo katika baraza hilo la kuwasilisha shughuli za utekelezaji wa maendeleo kipindi cha robo tatu ya mwaka 2021/2022.
Baadhi ya madiwani waliohudhuria baraza la kuwasilisha shughuli za utekelezaji wa maendeleo kipindi cha robo tatu ya mwaka.
Na Asha Mwakyonde,Bahi
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya Bahi Athman Masasi amesema kuwa wilaya hiyo imepata zaidi ya bilioni 5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwamo katika sekta ya elimu, maji, afya na miundombinu ya barabara.
Haya ameyasema leo Aprili 28, 2022 wilayani humo katika kikao cha siku mbili cha Baraza la Madiwani la kuwasilisha shughuli za utekelezaji wa maendeleo kipindi cha robo tatu ya mwaka 2021/2022, Mkurugenzi huyo amesema kuwa wamepata shule ya sekondari mpya iliyojengwa kwa gharama ya milioni 600 ambayo ipo katika hatua za mwisho.
Amesema kuwa shule hiyo inatarajiwa mapema mwaka huu kuanza kutoa huduma za kielimu na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande wa sekta ya afya ametoa fedha zaidi ya bilioni moja kuimarisha hospitali ya Wilaya.
Amefafanua kuwa fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa jengo la dharura lenye thamani ya milioni 300 na kwamba wanatarajia Mei 10, mwaka huu jengo hilo kuanza kufanya kazi.
"Nampongeza Rais Samia kwa kutupatia kituo cha afya katika Wilaya yetu, zaidi ya wananchi takribani 10,000 walikuwa wanapata shida katika huduma za afya lakini ameleta fedha zaidi ya milioni 250 ambazo na kituo hiki mwezi Mei kitaanza kutoa huduma kwa wananchi," ameongeza:
"Namshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuniamini na kunipa tena nafasi nyingine ya kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Bahi, na sisi kama Watendaji wake tunajivunia hatutamuangusha," amesema Mkurugenzi huyo.
Amesema kuwa kwa kipindi cha Rais Samia kazi zenye ubora zimefanyika kwa wananchi na kwamba fedha nyingi wamezipata za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza hilo Donald Mejiti amesema kuwa kila diwani anakuwa ameketi vikao katika kata yake na kujadiliana kuhusu changamoto na fursa ambapo wanawasilisha taarifa katika baraza hilo kwa kipindi cha robo mwaka.
Amesema kuwa sehemu kuwa ya taarifa za madiwani hao zimeonyesha mafanikio ya maendeleo kwa upande wa elimu,afya,maji, na miundombinu ambapo zaidi ya madarasa 72 yamejengwa kwa fedha za UVIKO-19.
"Tunaridhishwa na fedha zinazotoka serikali kuu na zile zinzotokana na mapato ya ndani tunazokusanya wenyewe," amesema mwenyekiti huyo wa baraza.
Ameongeza kuwa changamoto kubwa ni kutokuwa na mapato makuwa ya ndani na kwamba wanaendelea kubuni na kufungua fursa za kuongeza mapato.
Naye diwani wa Kata ya Bahi,Agustino Ndunu amesema yapo mafanikio makubwa katika kata hiyo ya miradi yote hususani miundombinu ambapo Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), tayari imeshatekeleza wajibu wao.
Diwani huyo ameeleza kuwa mafanikio mengine ni miundombinu ya maji ambapo tayari imeshasambazwa na imekamilika kwa asilimia 95 ipo katika hatua za mwisho na kwamba Wataalamu wake wapo vizuri.
"Suala la miundombinu kwa kata hii ipo vizuri hospital za Wilaya zaidi sita zipo katika hatua za mwisho na miradi mingine ya UVIKO-19 madarasa manne ya sekondari yameshakamilika na watoto wanasoma, madarasa mawili ya shule za msingi yameshakamilika na watoto wanapata elimu," amesema.
Ameongeza kuwa kuna changamoto ya barabara inayotoka makao makuu kwenda siginda na ile ya kati inayoenda kusini ambayo inatoka mwanachugu kuelekea sokoni nayo Inatakiwa kujenga kwa kiwango cha lami bado hawajapata fedha mwaka wa 2020/ 2021.
"Mwaka 2021/2022 hatujajua kama tutapata fedha na hii ni changamoto kwa barabara ya lami lakini pia kuwekewa taa kwani hapa Bahi ni mjini kuwe na taa kwa ajili ya usalama wa wananchi," amesema Ndunu.
Amefafanua kuwa kata hiyo ni kubwa inahitaji kuwa na soko ambalo linakidhi mahitaji ya wananchi wake.
Diwani Viti Maalumu Wilaya ya Bahi, Dominica Nyau amesema kuwa wanamafanikio makubwa katika Wilaya hiyo ikiwamo kuwa na viongozi mahidhiri ambao wanasimamia mapato ya ndani ya Halmashauri.
"Katika mapato hayo tunatumia kumalizia Zahanati mbalimbali katika Wilaya yetu, shule za msingi na sekondari pamoja na mambo mengine ya kimaendeleo ambayo yanahitaji fedha," amesema Diwani huyo.
Dominica ameongeza kuwa wanakabiliwa na changamoto za uelewa mdogo wa wananchi kujitokeza katika kuchangia nguvu kazi katika miradi ya maendeleo.
0 Comments