Kifaa cha kupimia ugonjwa wa shinikizo la damu
Na Asha Mwakyonde
DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),Dk.Sulende Kubhoja amesema kuwa kati ya watoto 100 wenye ugonjwa wa shinikizo la damu la juu (Hypertension), asilimia 70 wanatokana na tatizo la Figo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni daktari huyo amesema kuwa watoto wachanga wanaozaliwa ambao hawajamaliza siku 40 nao wanapata ugonjwa huo wa shinikizo la damu la juu.
Daktari huyo ameeleza kuwa watoto wanatofautiana umri katika kupata tatizo la shinikizo la damu la juu na kwamba ugonjwa huo kwa mtoto hawezi kugungulika hadi kufanyiwa vipimo.
" Hakuna namba maalumu kama ilivyo kwa watu wazima mfano 120 chini ya 80, kwa watoto inategemea na uzito wengine wanazaliwa na kilo gramu mbili na nusu, 3,4, hadi 5, kuna vitu vingi vinaangaliwa," ameeleza Dk. Kubhoja.
MFUMO WA MAISHA
Daktari huyo amefafanua kuwa kwa sasa katika taasisi hiyo wanaona kundi jingine la watoto kutokana na mfumo wa maisha kubadilika.
" Mtoto akiamka asubuhi anakaa kuangalia runinga (TV), anachezea simu ya kiganjani kazi za kujishughulisha hamna hachezi kwa sababu hakuna viwanja vikubwa vya kuchezea, shule anayoenda anapelekwa kwa gari anaongezeka uzito," amesema daktari huyo.
Ameongeza kuwa hilo nalo ni kundi jingine la watoto wanaopata ugonjwa wa shinikizo la damu la juu ndio mambo yanayotokea kwa watu wazima yanatokea kwa watoto hivyo anaweza hata kupata ugonjwa wa kisukari.
Dk. Kubhoja ameeleza kuna familia ambazo zinajulikana kuwa baba au mama ana shinikizo la damu la juu wanawaona watoto ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 wanapata tatizo la ugonjwa huo.
Amefafanua kuwa shinikizo la damu la juu haliji ghafla mara moja bali linakuja taratibu kama vile mwanadamu anavyokua hivyo basi kadri mtoto anavyokua anaongezeka uzito ndivyo ugonjwa huo unavyokua.
"Tunaweza sema ni mfumo wa maisha umesaidia kuchangia. Ukigundua mapema na maisha yakabadilika," amesema.
Ameongeza kuwa watoto ni Taifa la kesho hivyo wapimwe mara kwa mara ili kuepuka tatizo hilo kwani wanavyoenda hospitali kwa tatizo jingine ndio anagundulika na ugonjwa wa shinikizo la damu la juu.
0 Comments