WAOMBAJI AJIRA ZA SENSA WAFIKIA 119,468 KWA MUDA WA SIKU TANO

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati akitoa mwenendo wa maombi ya kazi za muda za makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi.

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MWENENDO wa uombaji wa maombi ya kazi za muda za makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi ambayo inatarajiwa kuanza Agosti 23 tayari serikali imepokea maombi hayo 119,468 nchi nzima.

Mei 5, mwaka huu serikali ilitangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya kazi hizo za muda wa Watanzania wenye sifa za kuomba.

Akizungumza leo  Mei 9, 2022 jijiji hapa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa amesema kuwa mwenendo wa maombi hayo unaendelea vizuri kupitia mfumo wa kielektroni na hadi kufikia  saa Saba mchana wa Mei 9, mwaka huu tayari wamepokea maombi hayo 119,468 kwa nchi nzima.

Mtakwimu huyo amefafanua kuwa kati ya waombaji hao  waombaji 46,159 ni waajiriwa kutoka katika sekta ya Umma na binafisi, waombaji 14, 393 wamejiajiri wenyewe  na waombaji 58,916  ni wale ambao hawana ajira.

Amesema kuwa baadhi ya changamoto ambazo waombaji wamekumbana nazo ni pamoja na waombaji  hao kutokujaza taarifa sahihi kama vile barua pepe na namba za simu hivyo kushindwa kupokea neno la siri na taarifa nyingine muhimu kumuwezesha muombaji kuendelea kukamilisha maombi yake.

Dk.Chuwa amesema kuwa changamoto nyingine ni waombaji hao kusahau jina la mtumiaji na neno la  siri hivyo kushindwa kuhuisha na kutuma fomu namba 1 iliyoidhinishwa  na mwajiri kwa waajiriwa na viongozi wa Serikali za Mitaa  pia kutokuwa na baadhi ya taarifa kama vile namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Ameongeza kuwa waombaji  kutokuwa na nyaraka za lazima za kuambatanisha kama vile cheti cha kuzaliwa na waombaji hao kuwa katika maeneo yenye mtandao hafifu hivyo kupata changamoto ya kutuma na kuhuisha maombi yao.

" Waombaji wote mnatakiwa kuwa makini wakati wa kuingia kwenye mfumo na usome ipasavyo kabla hujaanza kujaza  fomu namba 1 na kuhakikisha unafuata maelekezo,  na maombi yote ya kazi yatumwe kabla ya Mei 19 saa sita kamili usiku " amesema.

Aidha amefafanua kuwa Watanzania wote ambao hawana vyeti vya kuzaliwa fomu ya kiapo 'Affidavit' inaweza kutumika kama mbadala wa vyeti hivyo.


Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI