IGP SIRRO: TARI FIKENI VIJIJINI KUTOA ELIMU YA AFYA YA UDONGO


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro.

Na  Asha Mwakyonde

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro ameiomba Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),kutoa elimu ya afya ya udongo vijijini kwa kuwa taasisi hiyo ndiyo itakayookoa nchi kwani Watanzania wengi wanategemea kilimo kusomesha watoto wao.

IGP Sirro ameyasema hayo Julai 9,2022 wakati alipotembelea banda la TARI katika Maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Saba Saba yanayaofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, amesema sekta ya kilimo inachukua asilimia 70 hadi 80 ya Watanzania wanaolima.

Amesema  kwa umri wake ndani ya   serikali alionao hajawahi kusikia afya ya udongo huku akiomba TARI kufikisha elimu hiyo vijijini ili iwasaidie Watanzania isisubiri kutolewa katika Maonyesho ya biashara. 

" Watanzania wenzangu kwa umri huu ndani ya serikali nilionao siku ya leo ndio nimesikia afya ya udongo, hembu fikirieni mkulima anayekaa Butiama kijijini. Nilikuwa makini sana kusikiliza wakati Mkurugenzi Mkuu wa TARI anatoa maelezo ya afya ya udongo ndio maana nikajitolea mfano mimi mwenyewe,' amesema IGP Sirro.

Ameongeza kuwa kama mkulima wa kawaida hana elimu hiyo ni kazi bure, watu wengi wamesomeshwa kupitia kilimo hivyo elimu hiyo itolewe ili kuleta tija katika sekta hiyo.

"Wakati tunakua zamani chakula chetu kilikuwa ni mihogo ukienda kijijini ule mhogo haupo tena na ukiukuta ni mwembamba nilikuwa najiuliza tatizo lipo wapi? kumbe lipo kwenye udongo, amesema IGP Sirro.

Awali akitoa maelezo kuhusu taasisi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dk. Geofrey Mkamilo amesema kuwa wanaonyesha afya ya udongo ili mwekezaji yoyote kabla ya kuwekeza asipate hasara.

Dk. Mkamilo ameeleza kuwa jambo la kwanza mwekezaji lazima ajue kilimo ni Sayansi kuanzia afya ya udongo sio mtu yeyote anaweza kulima.

" Tunawatu mahiri wa masuala ya udongo, mwekezaji akishajua afya ya udongo itasaidia kujua kama anaweka mbolea ya aina gani, kiasi gani, kwa wakati gani, kwa mpangilio gani," amesema Dk. Mkamilo.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa wana vituo mahiri 17 nchi nzima vya  mazoa mahiri ya kimkakati kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa na chakula cha kujitosheleza pia kilimo kiweze kuchangia uchumi wa nchi.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU