WANACHAMA wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Dodoma, leo 31 Desemba 2025, wameishukuru Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa kuwapa mafunzo kuhusu udhibiti wa huduma za nishati na maji.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Musa Yusuf, ameipongeza EWURA kwa hatua ya kutoa mafunzo hayo, akibainisha umuhimu wa mkataba wa huduma kwa wateja, uvunaji wa maji ya mvua, na utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amesisitiza kuwa elimu waliyoipata wataitumia kwa kuelimisha umma.
“Asanteni sana EWURA kwa elimu hii, hakika imetufungua macho. Wenzangu wote ni mashahidi. Tunaomba mafunzo kama haya yaendelee,” amesema Bw. Yusuf.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Wilfred Mwakalosi, amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuelewa masuala yanayodhibitiwa na EWURA, kwani yanagusa huduma ambazo kila mwananchi kwa namna moja au nyingine anazitumia.
“Ninyi waandishi wa habari ni daraja kati ya EWURA na wananchi, tuendelee kushirikiana katika kuelimisha umma ili kila mtumiaji wa huduma tunazodhibiti ajue haki na wajibu wake”. Amesisitiza Mwakalosi.






0 Comments