Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Adolf Mkenda.
Baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Na WyEST Mwanza
MAKAMU wa Rais Dk.Phillip Mpango ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),vinaunganishwa na mkongo wa Taifa ili kuwezesha matumizi ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji.
Pia Dk.Mpango amewaasa Wahitimu wa Vyuo Vikuu kutumia vema elimu wanayopata kuleta tija kwa Taifa.
Dk. Mpango ameyasema hayo Novemba 24,2022 Jijini Mwanz wakati wa mahafali ya 41 ya Chuo hicho, amesema vituo hivyo vitaunganishwa na mkongo wa Taifa kwa lengo la kupunguza gharama uendeshaji.
"Vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria vitaunganishwa na mkongo wa Taifa na hili naagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha linafanyika mara moja jambo hili" ameongeza, Mpango
Awali akizungumza katika mahafali hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa. Adolf Mkenda, amesema Chuo Kikuu Huria kimetengewa fedha kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu, kusomesha wahadhiri na miradi mingine.
"Serikali kwa kutambua mchango wa Chuo Kikuu Huria katika kupeleka elimu kwa jamii kupitia mradi wa HEET tutajenga maabara saba katika mikoa ya Njombe, Arusha, Dodoma, Mwanza, Kigoma, Mtwara na Pwani ambazo zitajikita katika tafiti za kisayansi kulingana na shughuli na mahitaji muhimu ya eneo husika," amefafanua Waziri Mkenda.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kujenga vituo vya Chuo Kikuu Huria katika mikoa ya Geita, Kigoma, Lindi, Simiyu na Manyara ambao mikoa hii ilikuwa ikitumia majengo ya kukodi kwa gharama kubwa.
Zaidi ya Wahitimu 4,000 wametunukiwa Shahada mbalimbali zikiwemo Shahada Umahiri na Uzamivu wakiwemo wanafunzi kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ghana, Malawi, Zambia, Congo, Namibia na Ethiopia.
0 Comments