DARAJA LA KELEMA MAZIWANI NI MFUPA ULIOSHINDIKANA?


 Daraja la Kelema Maziwani ambalo limekatika tangu Aprili, mwaka 2020 huku likiendelea kutumika.

Barabara mbadala ambayo imetengenezwa katika mto ambao unajaa maji na kusababisha kuvunjika kwa daraja la Kelema Maziwani.

Na Asha Mwakyonde

LICHA  ya jidihada zinazofanywa na  serikali  ya Awamu ya sita za kuboresha miundombinu ikiwamo, madarasa, barabara na madaraja  lakini bado kuna baadhi ya maeneo yanachangamoto ya miundombinu hiyo.

Wilaya ya Chemba ni moja kati ya Walaya saba zilizopo katika Mkoa wa Dodoma ambazo ni Bahi,Chamwino, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa na Dodoma Mjini ambayo inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa  miundombinu ya daraja  lililopo kata ya Dalai katika Kijiji cha Kelema Maziwani.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Wilaya ya Chemba ilikuwa  idadi ya  wakazi  235,711 ambapo wanaume ni 117,585 na wanawake 118,126.
Dalai ni miongoni mwa kata  26 zilizopo katika Wilaya hiyo ambazo ni Chandama,Babayu,Chemba, Churuku,Goima,Farkwa,Jangalo,Kihama, Kwamtoro,Kidoka,Kinyamsindo, Lahonda,Lalta,Makorongo,Mondo, Mpendo,Mrijo,Msaada,Ovada,Paranga,Sanzawa,Songolo,Soya na Tumbakose.

Asilimia kubwa  ya wakazi wake ni kabila la Warangi, kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika  mwaka 2012 ilikuwa na watu 15,078.

Daraja la Kelema Maziwani ambalo lilijengwa mwaka 1966 na wakoloni
lililopo kijiji cha Kelama Maziwani katika kata hiyo  linalounganisha mikoa ya Tanga, Manyara, Dodooma na Manyara lilikatika tangu April 4, 2020 limekuwa ni kikwazo kwa wasafiri na hata wananchi 
wanaokizunguka Kijiji hicho kwa kukatika na kushindwa kupitika kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa.

Wananchi Kijiji cha Piho na maeneo ya jirani hutumia  daraja hilo kupita kwenda kupata huduma za afya katika zahanati iliyopo katika Kata Mondo pamoja na wanafunzi wanaoenda kusoma shule ya sekondari ya Mondo iliyopo katika Kata hiyo pamoja  na wanafunzi wa shule shule ya msingi hivyo kipindi cha mvua haipitiki  huduma za kijamii zina simama.

WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI

Wakizungumzia adha wanayoipata  kwa nyakati tofauti wakati wa mvua wanafunzi wa shule ya msingi wanaokaa kijiji cha Kelema Maziwani na kusoma shule ya msingi Piho wamesema kipindi cha mvua haendi shule kutokana na mto kujaa maji na  daraja hilo kutokupitika.

Mmoja wa wanafunzi hao anayesoma  darasa la tano katika shule ya msingi Piho Seleman Omar amesema mvua ikinyesha hawezi kwenda shule hali inayosababisha kukosa masomo  kutokana na daraja hilo kutopitika.

"Mvua ikinyesha siwezi kwenda shule mto huu unajaa maji na daraja hili kama unavyoliona ndugu mwandishi na hata hili la chini nalo maji yakijaa halionekani kabisa hivyo nalazimika kutokwenda shule hata zaidi ya Siku tatu hadi maji yapungue,"amesema mwanafunzi huyo.

 Mwanafunzi huyo  ameiomba serikali kufanya juhudi za  haraka kuhakikisha daraja hilo linajengwa.

Naye mwanafunzi  wa shule ya msingi Piho ambaye pia anaishi kijiji cha Kelema Maziwani Azeilina Mavere amesema wakati wa mvua kubwa haende shule anaogopa kupita katika daraja hilo.

"Baba yangu aliniambia mvua kubwa ikinyesha nisiende shule hadi mto utakapopungua maji, daraja hili ninbovu halipitiki kabisa kipindi cha mvua," amesema Azeilina.

WANAFUNZI WA SEKONDARI

Wakizungumzia changamoto ya kukosa masoma kipindi cha mvua wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mondo iliyopo kata ya Mondo ambao wanaishi Kijiji cha Piho wanasema wanakosa masoma jambo ambalo linawaumiza kisaikolojia pindi wanapofanya mitihani yao baadhi ya masomo wanafeli.

Mwanaidi Hassan ni mwanafunzi wa kidato cha kwa pili katika shule hiyo amesema hali ya daraja hilo la Kelema Maziwani sio nzuri hasa kipindi cha mvua halipitiki.

"Changamoto yetu ni kukosa masoma kipindi cha mvua hatuendi shule tunakosa baadhi ya masomo hali inayotusababishia tuonekane hatusomi pindi tunapofanya vibaya katika masomo yetu.

Kwa upande wake Bakari Ijengo amesema kitendo cha kukosa masomo kipindi cha mvua kinawasababisha wanapofanya mitihani kukutana na baadhi ya maswali ambayo hawakuingia darasani kutokana na kutokwenda shule hali inayowasababishia kufeli.


KAULI ZA WAZAZI

Kassim Mbaruku ni mmojwa wa wazazi ambao watoto wao wanasoma shule ya sekondari Mondo wanaoishi kijiji cha Piho amesema kipindi cha mvua  watoto hao wakichelewa kurudi wanapata 
wasiwasi kutokana na miundombinu mibovu ya daraja hilo.

Naye Mwanaidi Ninga ameiomb serikali kuharakisha ujenzi wa daraja hilo kwa kuwa ni muda mrefu tangu kukatika  huku akisema kumekuwa na watu tofauti tofauti kuja kufanya vikao lakini hakuna kitu kinachofanyika.

DIWANI 

Shaban Matereka ni diwani wa kata ya Dalai kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema kutokana na mvua nyingi zilizokuwa zinanyesha daraja hilo likizidiwa nguvu na maji ambopo lilikatika nguzo moja  tangu Aprili 2020.

Diwani huyo ameeleza kuwa Aprili 11, 2020  aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Saimon Odunga alitoa agizo la kufungwa daraja hilo.

"Agizo hili lilitekelewa kwa ajili ya Usalama zaidi wa wananchi,  tuliendelea kulizungumzia katika Baraza la madiwani  tukiomba meneja Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kweli walifika na kuendelea na mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu hadi ilipofika mwaka jana walikuja na kutuambia kuna kampuni  imeshinda zabuni kwa ajili ya kujenga daraja hili lakini hakuna chochote kinachoendelea,"ameeleza.

Diwani huyo amefafanua kuwa Tanroads waliwaomba kuitisha kikao cha watu 10  ambapo kijiji cha Kelema Maziwani walikuwa wanane na Piho watatu Katibu kata ,Diwani husika na diwani viti maalumu ambapo walifanya kikaao  na kampuni iliyoshinda zabuni.

"Tulipokutana na kampuni hii iliyoshinda zabuni wakatueleza lengo lao kuwa wanahitaji ushirikiano kutoka na wananchi na viongozi wa dini pamoja na watu wa mila na desturi ili kufanya ujenzi uende vizuri," amesema Matereka.

Amesema baada ya kikao hicho hawakurudi tena, walifike  watu wengine ambao walihitaji  mkutano wa hadhara kwa vijiji hivyo ambapo ulifanyika katika daraja hilo na kuelezea dhamira yao pamoja na kuomba sehemu ya kuhifadhia vifaa vyao pindi watakapoanza ujenzi.

Diwani huyo ameongeza kuwa baada ya mkutao waliahidi kwamba kipindi cha miezi kumi na sita daraja hilo litakuwa limekamilika, waliondoka na baadae walirudi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na kuchukua sampuli kwa kutumia mitambo yao lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea.

"Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alifanya ziara katika daraja hili, niliwasilisha hoja ya tatizo kuwa tataitzo la muda mrefu wananchi wanakwama kufanya  shughuli zao," ameongeza.

"Mkuu wa Mkoa alisisitiza ujenzi uanze na baada ya ziara hiyo baadae nilimfuata mbunge wangu Mohammed Moni akaniambia tayari wameshafanya thamini  na wameshaomba fedha za ujenzi wa daraja hilo ingawa sijajua ujenzi huu unaanza lini," ameeleza Matereka.

KAULI ZA WENYEVITI WA VIJIJI

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kelema Maziwani chenye wakazi 3478, Iddi Sokiro  amesema kuwa mara ya mwisho walifanya kikaao na mkandarasi ambaye alitakiwa kujenga daraja hilo Aprili mwaka huu na kwamba hadi sasa hawajui kinachokwamisha ujenzi huo.

"Kwa Sasa magari yanapita chini ambapo kumewekwa mkeka wa zege ni hatari pia kipindi cha mvua nashukuru kwa kututafuta tunaomba utusaidie kupasa sauti ili daraja hili lijengwe limekuwa ni kero mno kwa wananchi na wanafunzi," amesema Sokiro.

Ameeleza kuwa gharama iliyotumika kujenge, kutengeneza barabara mbadala ya chini  inaonekana ni kubwa ambapo serikali ingeweza kuongeza fedha na kujenga daraja hilo huku akisema suruji iliyotumika ni zaidi ya mifuko 2000 na nondo kati ya tani moja na Nusu hadi mbili.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Piho chenye wakazi 600,  Ikrami Mohammed amesema huu ni mwaka wa tatu tangu kukatika kwa daraja hilo ambalo linakwamisha shughuli za kijamii zikiwamo huduma za afya, elimu kwa wanafunzi na wafanyabiashara.

"Siku mvua ikinyesha kubwa watu hawataendi  mshabani wanafunzi hawataenda shule na wagonjwa hawataenda hospitali  ni hatari shughuli mbalimbali za kijamii sinasimama kutokana na miundombinu mibovu ya daraja hili," ameeleza.

Ametolea mfano mvua ikinyesha wiki nzima  wanafaunzi wataathirika kimasomo na kwamba siku ya mitihani atakuna na swali ambalo hakuwahi kusoma kutokana na kushindwa kupita.

TANROADS

Salehe Juma ni Mhandisi wa Mipango kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads),amesema kuwa wapo katika usanifu wa kina na kwamba utakapokamili ujenzi wa daraja hilo utanza.

"Usanifu wa kina bado haujakamilika tutakapo kamilisha ndio tutaanza utaratibu wa ujenzi wa daraja hili,"ameeleza Mhandisi huyo wa Mipango.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI