UKOSEFU WA VIVUKO UNAVYOSABABISHA WAKINAMAMA KUJIFUNGULIA PEMBENI YA MAKORONGO


 Na Asha Mwakyonde

SERIKALI imekuwa ikihakikisha miundombinu mbalimbali inaboreshwa  ikiwamo madarasa, madawati na barabara lengo ni kuhakikisha wananchi hawapati vikwazo katika shughuli zao  na wanafunzi wanapata elimu bora.

Licha ya serikali kuendelea kuboresha miundombinu lakini kuna baadhi ya miundombinu hiyo amboyo haipewi kupaumbele na ni changamoto kwa wananchini.

Chemba ni moja ya wilaya saba zilizopo katika Mkoa wa Dodoma ambayo ilianzishwa mwaka 2012 baada ya kumegwa kutoka wilaya ya Kondoa.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Wilaya ya Chemba ilikuwa na idadi ya wakazi 235,711 ambapo wanaume ni 117,585 na wanawake 118,126.

Kata ya Mondo ina vijiji vinne ambayo ni Pongai, Waida, Daki na Mondo yenyewe ambayo iilikuwa na idadi ya wakazi 9494 waishio humo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.

Vijiji viwili vya Daki na Waida vinakabiliwa na changamoto ya makorongo ya mito ambayo inajaa maji kipindi cha mvua na kusababisha wananchi na wanafunzi kushindwa kupata huduma za kijamii kwa wakati kama kufika shuleni na katika huduma za afya.

Huduma za afya na shule ya sekondari ya Mondo zinapatikana upande wa pili wa makorongo hayo jambo linalosababisha  wananchi na wanafunzi wa vijiji hivyo kukabiliwa na changamoto ya kuvuka kipindi cha masika.

WENYEVITI WA VIJIJI

Wakizungumzia kero na changamoto wanazozipata wananchi wao kwa nyakati tofauti wenyeviti wa vijiji vya Daki na Waida wamesema kuwa tayari makorongo hayo yalishasababisha kifo cha mwalimu mmoja miaka ya nyuma pamoja na mama mjazito aliyekuwa ana umwa uchungu kushindwa kuvuka ambapo alijifungua akiwa anasubiri maji yapungue ili avushwe.

Mohammed Kayaga maarufu Maine ni Mwenyekiti wa kijiji cha Waida amesema kuwa mkazi wake aliwahi kujifungulia kando ya korongo la Kwa Hobe wakati akisubiri maji yapungue ili wavuke kwenda katika Zahanati ya Mondo.

"Walifika saa nne asubuhi wakatuka mto umejaa, korongo limejaa maji wakati wanasubiri maji yapungue mama yule mjamzito alijifungulia hapa hapa pembeni ya hili korongo ni hatari sana mtu anaweza kumpoteza mtoto wake," amesema.

Ameongeza kuwa kipindi cha masika wanafunzi wanashindwa kupita,wanatoka saa kumi na moja na nusu alfajiri ambapo wakikuta mto umejaa wanasubiri maji yapungue na wakati mwingine wanachelewa kufika shuleni au wanashindwa kuwenda wanapoteza masomo yao.

Mwenyekiti huyo ameeleza kipindi cha uchaguzi wanasiasa, wabunge na madiwani wamekuwa wakitumia makorongo hayo kuombea kura kwa wananchi na kuahidi kuweka vivuko na kwamba wakipata nafisi hizo hawakumbuki kutimiza ahadi hiyo.

"Sielewi gharama ya kuweka vivuko au kujenga kalavati ni kubwa au ala ndio maana serikali inashindwa kutenga bajeti ya vivuko hivyo? ," amehoji mwenyekiti huyo.

Kayaga amesema kuwa kwa mtazamo wake kama serikali imeshindwa kuwasaidia washirinane vijiji vitatu ambavyo ni Waida,Daki na Mondo ili wajenge vivuko kwa nguvu za wananchi.

Naye Bunge Tesa ni Mwenyekiti wa kijiji cha Daki ameeleza kuwa Wana njia,barabara zenye makorongo yanayopitisha maji wakati wa mvua wanafunzi wanakaa kusubiri maji ya pungue hadi saa nne ndio waweze kupita huku wenzao wakiwa wanaendelea na masomo.

Ameongeza kuwa kwa hali hiyo mwanafunzi hawezi kupata elimu inayotarajiwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia amesema wakiwa na mgonjwa kipindi cha mvua hawaweze kuvuka kumpeleka katutokana na Zahanati ya Mondo kuwa ng'ambo upande wa pili na badala yake wanatumia dawa za kienyeji yaani tiba mbadala. 

"Miaka ya hivi karibuni kuna mwalimu alikuwa akiishi hapa kazi anafanyia kata ya jirani Dalali alipotezamaisha kwa kusombwa na maji kipindi cha masika ni hatari sana katika makorongo haya," amesema.

WANANCHI WA VIJIJI HIVYO

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao wa vijiji hivyo Josephat Iyuda, Elizabeth Damian wamesema kati ya mwaka 2000 na 2001 mwalimu wa shule ya msingi Dalai ambaye walimtaja kwa jina moja kimolo alipoteza maisha kwa kusombwa na maji.

Iyuda mkazi wa kijiji cha Daki kitongoji cha Daki juu ameeleza kuwa mchangamoto iliyopo ni mvua ikinyesha kubwa wanafunzi na wagonjwa hawahawezi kuvuka na bahati mbaya mgojwa akizidiwa atapoteza maisha kabla hajafikishwa katika Zahanati ya Mondo iliyopo kijiji cha pili Mondo.

Ameongeza kuwa katika kijiji hicho kuna vivuko vitatu ambavyo ni Kwa Hobe, kwa Jumbe na Pampuka na kwamba vivuko vyote hivyo vinatumiwa na wanafunzi pamoja na wakazi wa kijiji hicho.

Naye Elizabeth Damian mkazi wa kijiji cha Daki amesema kuwa wanapata shida akina mamawajawazito na wanafunzi pamoja na wagonjwa na kwamba kipindi cha masika hawana njia nyingine ya kupita ili wakapate huduma muhimu za kijamii.

"Tuna changamoto moja kubwa ya vivuko kipindi cha mvua ni hatari huduma za kijamii tunashindwa kuzifikia kwa wakati mfano mama anapoumwa uchungu hawezi kwenda hivyo hujifungulia nyumbani,"amesema.

Naye mkazi wa kijiji Cha Waida Aziza Matula ameeleza kuwa huduma zote zinapatikana katika kijiji cha Mondo hivyo kipindi cha masika ni changamoto kwao.

"Ndugu mwandishi unajua kuwa hata tukitaka kusafiri lazima tufike Mondo ndio barabara kuu, huduma za afya na shule ni huko huko, tuna changamoto nyingi tumesahaulika lakini ikifika kipindi cha uchaguzi unawaona wanasiasa wanavyokuja kujinadi na kutuahidi mambo mazuri ikiwamo kutujengea vivuko lakini tukiwapa kura hatuwaoni," amesema.

OMBI KWA SERIKALI

Wakazi hao wanaiomba serikali kuwakewa vivuko vya muda ili waweze kupita kwa urahisi kwa kuwa huduma za kijimii zikiwamo shule, Zahanati na soko zinapatikana kijiji cha Mondo upande wa pili.

KAULI ZA WANAFUNZI

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi ambao wanasoma katika shule ya sekondari ya Mondowamesema kuwa mvua ikinyesha hawawezi kwenda shuleni kutokana na makorongo hayo kujaa maji.

Zaidani Bashir ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo kutoka kijiji cha Waida amesema wanapata shaida kipindi cha mvua kuvuka korongo la Kwa Hobe jambo ambalo linawaathiri katika masoma yao pindi wanaposhindwa kuvuka korongo hilo.

"Tukikuta korongo limejaa maji tunasubiria maji yapungue na muda mwingine viatu vyetu vinaondokana maji, mvua ikiwa kubwa hatuwezi kwenda shule tunabaki nyumbani wenzetu wanaendelea na masomo," ameeleza mwanafunzi huyo.

Kwa upande wa Airon Seleman mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo anayeishi kijiji cha Daki amesema kuwa pamoja na kuchelewa wakati wakisubiri maji yapungue katika makorongo hayo wanapata adhabu ya kuchapwa na baadhi ya walimu.

"Kipindi cha masika huwa tunakosa masoma na tukienda kwa kuchelewa mwalimu mwingine anaweza akatuadhibu na mwingine akatusamehe, tusipofika shuleni wenzetu wanaendelea na masomo. Siku mvua ikinyesha mfulilizo nasi hatuendi shule tunapofika tunakuta wenzetu wapo mbali wamesoma topiki hata tatu kwa somo moja," amesema mwanafunzi huyo.


WITO WAO KWA SERIKALI

Wanaiomba serikali kuwawekea kivuko ili waweze kupita hata kipindi cha mvua waweze kuendelea na masoma yao Kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.

Pia wameomba kujengewa mabweni ili kuondokana na adha ya makorongo wanayopita kipindi chamasika lengo likiwa ni kutopoteza baadhi ya vipindi wanavyokosa wakiwa nyumbani baada ya kushindwa kuvuka makorongo hayo.

WAZAZI WA WANAFUNZI

Mkazi wa kijiji cha Daki Arafa Iddi mzazi wa mwanafunzi Abdul Ramadhani ambaye anasoma kidato cha kwanza katika shule hiyo amesema wao kama wazazi wanahofu kubwa kipindi cha mvua watoto wao wanapoenda shule.

Ameongeza kuwa mbali na wanafunzi hao kuvuka makorongo hayo akinana mama wajawazito wanapoumwa uchugu kipindi cha mvua wengi hujifungulia njia, nyumbani hali inayosababisha athari kwa afya ya mama na mtoto.

Iyuda ambaye pia ni mzazi amesema kuwa mvua inaweza kunyesha siku tatu,walimu shuleni wanaendelea kuwafundisha waliopo darasani ambao hawatoke maeneo yenye changamoto, vikwazo.

"Kimasimo wanaathirika kwa kutohudhuria baadhi ya masomo kadhaa na hata wakipewa notisi inakuwa haimsaidii mwanafunzi kuelewa," ameeleza mkazi huyo.


KAULI YA TARURA

Akizungumzia mchakato wa makorongo hayo Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),kutoka Wilaya ya Chemba, Mhandisi Matias Makaju amesema kuwa barabara ambayo ipo kwenye utaratibu wao ni ile ya Pampuka inayoenda hadi kijiji cha Waida.

"Kwenye taratibu zetu kama Tarura tumeshaiandikia kuomba hela, kwenye vipaumbele na kuchakata tunasubiri, kwa uhalisia wake hapa kuweka daraja inaweza kuchukua zaidi ya robo hela yake kuweka hapo, hivyo tumeiombea hela na tayari tumeshafanya utafiti hivyo tunasubiria," amesema.

Amesema kuwa barabara inayotoka Mondo kati inayopita shule ya sekondari kuelekea Daki katikakorongo la Kwa Jumbe barabara hiyo haijauiwishwa hivyo haijaingizwa kwenye taratibu za matengenezo.

Mhandisi huyo amefafanua kuwa bado wanafanya upembuzi yakinifu na wakiona kuna haja ya kuweka vivuko watawashirisha viongozi husika wa Halmashauri ili kuweza kuombea hela na kuweka vivuko hivyo.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI