WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan yupo mstari wa mbele mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.
Pia Waziri Mhangama amezindua 'programu Rafiki' yenye lengo la kutatua kero na kuzitafutia ufumbuzi ambayo itawasaidia wananchi kuichukia rushwa.
Akizungumza jijini hapa Disemba 20,2022 wakati akifungua Mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru,wenye kauli mbiu isemayo 'Kuzuia Rushwa ni Jukumu lako na langu:Tutimize wajibu wetu, waziri huyo amesema kuzuia rushwa ni bora kuliko kupambana nayo.
Waziri Mhangama amesema faida ya kuzindua programu ya Rafiki ni kubwa inakwenda kujenga utayari kwa wananchi na kwamba itasaidia kuwasababishia Watanzania wote kuchukia vitendo vya rushwa na madhara yake.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Kamishna (CP), Salum Rashid Hamduni ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni
Kuokolewa kwa jumla ya Shilingi Bilioni 14.3 (14,272,889,626.76) na Dola za Marekani 14,571 (Sawa na Shilingi 34,970,400), kupitia operesheni mbalimbali za TAKUKURU na kudhibiti vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2017/18 - 2021/22.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa malengo yaliyowekwa na Taasisi hiyo kwa mwaka huo katika majukumu ya Uzuiaji Rushwa, Uelimishaji Umma, Uchunguzi na Huduma za Sheria, ulifikiwa kwa wastani wa asilimia 89.4 ya malengo iliyojiwekea kwa Mujibu wa Mpango Mkakati wa Takukuru ambapo Utekelezaji huo ni ongezeko la asilimia 1.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 87.7 uliofikiwa mwaka 2020/21.
"Mafanikio haya pia yanaonekana kupitia matokeo ya Utafiti wa kitaifa kuhusu hali ya Utawala na Rushwa wa mwaka 2020, ambapo asilimia 78 ya wahojiwa katika Utafiti huu, wameonesha kuwa rushwa ipo kwa kiwango cha chini, na asilimia 87.7 walionesha kuwa rushwa imepungua," amesema.
Ameongeza kuwa hiyo imetokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika kufanikisha malipo na utoaji wa baadhi ya huduma na kwamba mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa yanabainishwa katika vipimo vya kimataifa kuwa wamepiga hatua.
Mkurugenzi huyo Amefafanua kuwa Mathalan, Transparency International kupitia taarifa yake kuhusu kiashiria cha rushwa (Corruption Perception Index) mwaka 2021, inaonesha kuwa Tanzania imepata alama 39 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180, ikiwa imepanda kutoka alama 30 na nafasi ya 119 mwaka 2015.
Amesema kwa muktadha huo, Tanzania imeorodheshwa kati ya nchi sita zilizopiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa barani Afrika, nchi nyingine ni Angola, Ethiopia, Rwanda, Ivory Coast, Senegal na Shelisheli.
Kamishna huyo ameeleza kuwa Kiashiria kingine cha The Rule of Law Index cha World Justice Project (WJP) kimebainishwa kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua na kuonesha kufanya vizuri kwa mwaka wa tatu mfululizo katika kukabiliana na vitendo vya rushwa hususan, kwa kuzuia hongo, matumizi mabaya ya madaraka na ufujaji katika mihimili ya Utawala, Mahakama na Bunge kwa kupata alama 0.46 na kushika nafasi ya 98 kati ya nchi 140 duniani.
"Kwa mujibu wa taarifa hii, Tanzania ni nchi ya pili kwa nchi za Afrika ya Mashariki na inashika nafasi ya 12 kati ya nchi 34 za kusini mwa Jangwa la Sahara.Kutokana na juhudi za Serikali na mafanikio haya, " amesema.
0 Comments