📍Wazabuni watakiwa kupata
Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MAMLAKA ya Rufani ya Ununuzi wa Umma (PPAA) imewataka wazabuni na wadau wote wa ununuzi wa umma nchini kushiriki mafunzo ya matumizi ya moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) ili kuongeza ufanisi na uelewa wa matumizi ya mfumo huo.
Wito huo umetolewa leo Feburari 25, 2026 jijini hapa na Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
kutangaza miradi ya maendeleo na fursa za vijana kwa mwaka 2025/2026, amesema mafunzo hayo yatakapokuwa yanatangazwa na mamlaka hiyo, ni muhimu kwa wazabuni kushiriki ili waweze kuelewa namna bora ya kutumia moduli hiyo wanapokabiliwa na changamoto katika michakato ya ununuzi wa umma.
Amefafanua kuwa kupitia moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST, PPAA imefanikiwa kuunganisha taasisi nunuzi zote nchini katika mfumo mmoja unaomwezesha mzabuni kuwasilisha rufaa yake kwa taasisi husika kwa njia ya kielektroniki.
“Baada ya kuwasilisha rufaa, Mamlaka ya Rufani ina uwezo wa kufuatilia na kuona nyaraka zote zinazotumika katika mchakato mzima wa zabuni inayolalamikiwa,” amesema Sando.
Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni kuunganisha moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa na mfumo wa mahakama, zoezi litakalotekelezwa katika mwaka wa fedha ujao kwa lengo la kuongeza uwazi na kuharakisha upatikanaji wa haki.
Kwa mujibu wa Sando,lengo la kuunganisha mifumo hiyo ni kutoa huduma bora, stahiki na kwa wakati kwa wananchi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na maelekezo ya Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika utoaji wa huduma.
Amesema dira hiyo imeweka mkazo katika matumizi ya TEHAMA ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa haraka, kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.
Sando amesisitiza kuwa PPAA itaendelea kuchukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kuboresha mifumo ya utoaji haki katika michakato ya ununuzi wa umma na kuimarisha utawala bora nchini.



0 Comments