WANAKIJIJI WATOA EKARI 65 KWA AJILI YA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI


Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Saidi Mchome, akiwapa maelekezo wanakamati ya ujenzi wa shule ya sekondari ambayo inatarajiwa kujengewa katika kijiji cha Kelema Maziwani baada ya kupima sehemu ya ujenzi wa vyoo.

Na Asha Mwakyonde, Chemba

ZAIDI ya wakazi 30 wa kijiji cha Kelema Maziwani kilichopo  Kata ya Dalai, Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma wametoa ekari  65  kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ambapo kwa sasa wanafunzi wa kijiji hicho wanatembea umbali wa kilometa tano kuifikia shule ya sekondari ya Mondo iliyopo kata ya Mondo Wilayani hapo.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa kijiji cha Kelema Maziwani, mkazi wa kijiji cha Daki, Kata ya Mondo, Mary Kimolo ambaye ana shamba katika hicho,  amesema kuwa waliitwa na  kuombwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya kujenga shule hiyo.

Ameongeza kuwa baada ya mazungumzo marefu baina yao wenye mashamba na uongozi wa kijiji hicho walikubali kupisha maeneo yao kwa makubaliano ya kubadilishiwa ambapo wamepewa shamba la kijiji ili waendelee na shughuli zao za kilimo.

 
Mary ameeleza kuwa tayari Ofisi ya kijiji hicho ilishamuita mtu wa ardhi ambapo walipimiwa mashamba yao na kwamba zoezi hilo limekamilika bila kutokea mgogoro wowote.

" Tulifurahi kwa kuwa ni suala la maendeleo tuliamua kukubali kwa pamoja kwani watoto wanachoka kutembea umbali wa kilometa tano kwenda na kurudi wanatembea kilomita 10 kwa siku," amesema mkazi huyo.

Mwenyekiti wa kamati ya Ujenzi  na Mjumbe wa serikali ya kijiji hicho  Issa Isambi  amesema lengo kuu walilo nalo wanakijiji wa Kijiji hicho cha Kelema Maziwani pamoja na vijiji vya Piho, Mondo, Waida na Pongai ni kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu wanafunzi wanaotoka katika vijiji hivyo.

"Tunashukuru serikali kwa kukubali ombi letu na sisi tupo tayari kutumia nguvu kazi zetu ili kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unakamilika na kufikia lengo letu. Na ni matumaini yetu serikali itamalizia ujenzi ili kukamilisha madarasa, " amesema Isambi.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Dalai Shaban Matereka amewashukuru  wananchi wa kijiji hicho na baadhi ya wanakijiji wa Kata ya Mondo kwa kuwa wameamua kutoa mashamba yao ili kupisha ujenzi wa shule ya sekondari.

"Tupo hapa katika eneo ambalo tunakusudia kujenga shule ya sekondari ambayo itawapunguzia wanafunzi kutembea umbali wa kilometa tano wanaotoka vijiji vya Piho, Pongai, Waida na Kelema Maziwani yenyewe. Kutoa eneo sio kazi rahisi kwani walishayazaoe lakini wameamua ili kujanga huduma za kijamii," ameeleza diwani huyo.

Akizungumzia hatua za awali  Afisa Mtendaji wa Kata ya Dalai Asha Kaita ameeleza kuwa hatua hizo za awali  zimeshaanza kufanyika  kwa kupima maeneo ya kujenga vyoo ambapo ujenzi utaanza  kwa kutumia nguvu za wananchi wa kijiji hicho.
 
"Tuliwaita wananchi kwenye kikao na kuwashirikisha, walikubali  kuwa kijiji hiki kina shamba la Ujamaa walikubali kwenda kwenye shamba hilo na wao pia wanapenda maendeleo," amesema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Iddi Sokiro amesema kuwa eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na wananchi kwa hiari yao baada ya vikao baina ya wananchi hao na uongozi wa Kata pamoja na uongozi wa kijiji walikubali kupisha ujenzi wa shule.

Mhandisi wa  Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Saidi Mchome, amewapongeza wananchi ambao wamejitolea kutoa maeneo huku akisema wameonesha nia ya kuhakikisha wanapata shule ili kuwanusuru wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Mhandisi Mchome amesema kuwa amepima eneo la vyoo lenye matundu 12  ambapo wanawake  matundu sita na wanaume pia idadi ni ya  matundu sita.

"Katika ujenzi huu kwa sasa inabidi wananchi hawa waanze kwa kutumia nguvu zao baada ya hapo serikali itaangalia namna kuleta madarasa ili shule isajiliwe inatakuwa kuwa na madarasa nane," ameeleza Mhandisi Mchome.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU